Raphael Dwamena, tayari alikuwa ameifungia klabu yake mabao tisa msimu huu unaoendelea. Picha: Getty 

Raphael Dwamena, mwenye umri wa miaka 28 anayechezea klabu ya FC Egnatia FC ligi ya Albania, alijiunga na klabu hiyo Desemba mwaka 2022 na tayari alikuwa ameifungia klabu yake mabao tisa msimu huu unaoendelea.

Klabu ya Egnatia FC imethibitisha kifo cha nahodha wake Dwamena huku ikitoa risala za rambirambi kwa niaba ya rais wa timu hiyo Agim Demrozi.

"Dakika ya 25 ya mechi dhidi ya Partizan ilikuwa wakati wa hofu kwetu sote wakati nahodha wetu Raphael Dwamena alianguka chini na kutuacha sote vinywa wazi. Tunatuma salamu za pole kwa familia ya marehemu kapteni Raphael Dwamena" Klabu iliandika.

"Licha ya huduma ya kwanza kutolewa na madaktari wetu uwanjani na pia katika hospitali ya Rrogozhina, Dwamena hakufanikiwa kuokolewa."

Raphael Dwamena wa Ghana akishindania mpira na Matt Hedges wa Marekani wakati wa mechi ya Kirafiki ya Soka ya Kimataifa kati ya Marekani na Ghana, katika Uwanja wa Pratt & Whitney mwaka 2017.

Pia, shirikisho la soka la Ghana, limetoa taarifa likieleza kusikitishwa na kifo cha mwanasoka wake wa zamani Raphael Dwamena huku likituma salamu za rambirambi kwa familia ya mechzaji huyo katika wakati huu mgumu.

"Habari hii ni ngumu kupokea. Tunaitakia pole familia yake kwa wakati huu. Aliitumikia nchi yake vizuri na alionyesha ubora kila wakati alipowakilisha Ghana" Rais wa shirikisho la soka Ghana Simeon-Okraku alisema.

Dwamena alicheza Levante, Red Bull na FC Egnatia ya Albania.

Klabu yake ya zamani ya Levante nchini Uhispania, pia ilituma rambirambi zake.

"Kwa niaba ya Levante UD, tungependa kutoa rambirambi zetu kwa kifo cha mchezaji wetu wa zamani, Raphael Dwamena." Iliandika kwenye mtandao wa X.

Dwamena aliiwakilisha timu ya taifa ya soka ya Ghana katika mechi 9 huku akifunga mabao 2.

TRT Afrika