Viongozi wa Ligi Kuu nchini Hispania, Barcelona wamepoteza mchezo wao wa ugenini dhidi ya Monaco ya Ufaransa, baada ya kukubali cha mabao 2-1 kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Ulaya (UEFA), uliochezwa Septemba 19, 2024.
Mabingwa hao wa zamani wa La Liga, walimaliza mchezo huo wakiwa pungufu, baada ya beki Eric Garcia, kuoneshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Takumi Minamino, aliyekuwa akielekea kufunga.
Maghnes Akliouche aliitanguliza Monaco mbele katika dakika tano ya mchezo kabla ya kinda wa Blaugrana, Lamine Yamal kuisawazishia Barcelona katika dakika ya 28, baada ya kuachia kombora kali kutoka wingi ya kulia kutumia mguu wake wa kushoto.
Monaco iliongeza bao lake la pili kupitia kwa George Ilenikhena, na kuwawezesha timy hiyo kuvuna alama tatu nyumbani.
"Mchezo ulibadilika kabisa baada ya dakika 10 kutokana na kadi nyekundu, lakini ninachoweza kuona ni kitu chanya," kocha wa Barcelona Hansi Flick aliwaambia waandishi wa habari.
"Tulijaribu kuweka ulinzi kama timu na pia kushambulia, na tulipata nafasi, lakini wanastahili ushindi, kwa hivyo lazima tukubali hilo."
Nchini Italia, kipa wa Arsenal, David Raya aliipatia timu yake pointi moja muhimu katika mwanzo mgumu wa kampeni ya klabu hiyo dhidi ya Atalanta kwa kutoka sare ya 0-0.
Atalanta ilipata penati baada ya Thomas Partey kumchezea vibaya Ederson, hata hivyo Raya alipangua mchomo uliopigwa na Mateo Retegui.
"Ni penalti tu na nilikuwa na bahati ya kwenda njia sahihi na kuokoa," Raya aliambia TNT Sports.
Kwengineko, nyota wa Ujerumani na Bayer Leverkusen, Florian Wirtz alifurahia kutimiza ndoto yake ya mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa wakati mabingwa hao wa Bundesliga walipoichabanga Feyenoord ya Uholanzi 4-0 ugenini. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alitupia mabao mawili.
Klabu ya Atletico Madrid ya Hispania ilishinda 2-1 nyumbani, dhidi ya RB Leipzig ya Ujerumani, na kuvuna alama tatu muhimu, kupitia bao la dakika za majeruhi lililofungwa na Jose Maria Gimenez.
Michuano ya Ligi ya Mabingwa itarejea tena Oktoba 1 na 2 wakati Arsenal itakapoikaribisha Paris Saint-Germain ya Ufaransa, huku Bayern Munich wakisafiri hadi nchini Uingereza kupambana na Aston Villa wakati mabingwa watetezi Real Madrid wataifuata Lille huko Ufaransa.