Ali alikuwa bingwa asiyepingika wa uzito wa juu wa dunia / Picha : Getty 

Bingwa wa masumbwi duniani Mohammed Ali ametangzwa kujumuishwa katika orodha ya mabingwa Hall of Fame ya wamiliki wa mieleka WWE nchini Marekani.

"Wengi wanadai kuwa bora, lakini ni mwanamume mmoja tu ndiye 'The Greatest," aliandika Tripple H, mkurugenzi wa kampuni ya mieleka ya WWE, katika mtandao wake wa X.

"Muhammad Ali alishinda mchezo na kuwa mwanariadha wa kimataifa ambaye alivutia na kuathiri ulimwengu kama vile hakuna mwingine. WWE inaheshimika kumjumuisha ‘Bingwa Mkuu’ Muhammad Ali katika #WWEHOF,” aliongeza.

Katika taarifa, WWE ilisema: "akitambulika kuwa bora zaidi, ushawishi wa Ali ulivuka michezo mbali mbali na hata nje ya michezo kwani kazi yake kama mwanaharakati, msanii, na haiba yake kijumla ilimfanya kuwa mmoja wa watu mashuhuri zaidi ulimwenguni."

Japo Mohammed Ali hakuwa mwana mieleka, aliwahi kupigana katika pambano na mwanamieleka wa Kijapani Antonio Inoki, lililofanyika kwenye uwanja wa Nippon Budokan huko Tokyo, Japan, Juni 26, 1976.

Ali alikuwa bingwa asiyepingika wa uzito wa juu wa dunia wakati huo, lakini hii haikuwa mechi ya ndondi ya kawaida na wala haikuwa pia mieleka ya kawaida.

Kwa hiyo Kulikuwa na mchanganyiko wa mangumi na mateke. Inoki alimshambulia Ali kwa mateke miguuni na hivyo kumzuia Ali kumfikia kwa mangumi. Hatimaye Inoki anadaiwa kumpiga Ali mateke 64 huku Ali akiangusha ngumi 5 pekee.

Majaji waliamua kuwa pigano hilo lilitoka sare kwa usawa wa alama.

Mohammed Ali ni miongoni mwa majina makubwa zaidi katika historia ya masumbwi duniani./ Picha : Getty 

Hii sio mara ya kwanza kwa mtu nje ya mieleka kujumuishwa katika Hall of Fame ya WWE.

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, Mwana masumbwi mwingine Mike Tyson na muigizaji William Shatner wamewahi kupewa hadhi hiyo.

Sherehe hiyo inatarajiwa kufanyika tarehe tano Aprili katika kituo cha Wells Fargo mjini Philadelphia. Wengine watakao jumuishwa katika hafla hiyo kitengo cha 2024 ni Paul Heyman, Bull Nakano, Mike Rotunda na Barry Windham.

Mjane wake Mohammed Ali, Lonnie Ali atasimamia shughuli hiyo okwa upande wa familia yake.

Mohammed Ali ni miongoni mwa majina makubwa zaidi katika historia ya masumbwi duniani.

Alifariki 2016 akiwa na miaka 74.

TRT Afrika