Ufanisi wa Angella Okutoyi kwenye tenisi umevutia ufuasi mkubwa kwenye mchezo huo. / Picha: AFP

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 19, alimshinda Isabella Harvison wa Marekani 2-0 (6,2 7,2) katika fainali na kuwa Mkenya wa pili katika historia ya tenisi tangu Paul Wekesa mwaka 1994, kushinda taji la tenisi la kitaalam kwa mchezaji mmoja.

Hata hivyo safari ya Angella Okutoyi kutwaa kombe hilo la Monastir nchini Tunisia haikuwa rahisi kwani alijizatiti na kumlaza Mfaransa Yasmin Mansouri kwenye raundi ya pili kwa ushindi wa seti 6-4, 6-0 na baadaye kumchuja Anastasia Abbagnato wa Italia 6-2, 1-6, 6-1 katika hatua ya robo fainali.

Alipotua nusu fainali, Angella hakuchelewa kumtesa na kumtoa Zeel Desai wa India 6-1, 7-6 na kuweka historia kwa kutinga na hatimaye kutwaa taji la ITF W15 Monastir.

Jina la nyota huyo limewekwa kwenye orodha ya washindi ya Wimbledon baada ya kuweka historia mnamo 2022, kwa kuwa Mkenya wa kwanza kushinda taji la Grand Slam pamoja na mshirika wa Uholanzi Rose Marie Nijkamp wakishinda taji la wasichana la Wimbledon kwa wachezaji wawili. Matokeo hayo yalimvutia Angella sifa kutoka nyota mbalimbali akiwemo Lupita Nyong'o.

Angella alitumia ukurasa wake rasmi wa mtandano na kuandika, "Unajua wanachosema … KAZI NGUMU INA MALIPO !! TAJI YANGU YA KWANZA YA PRO W15 na sio ya mwisho !!.

"Tenisi Kenya inajivunia sana Angella na bidii na uthabiti ambao ameonyesha," Katibu Mkuu wa Tenisi Kenya Wanjii Mbugua-Karani, amesema.

Katibu Mkuu wa Tenisi Kenya Wanjii Mbugua-Karani. / Picha: AFP

Wanjii ameongeza kuwa ufanisi wa Angella utahamasisha ushiriki katika mchezo huo na kuiinua kiwango cha tenisi nchini Kenya.

TRT Afrika