Klabu ya Nice ya Ufaransa yamsimamisha beki wa Algeria kwa chapisho la utata juu ya Israel-Gaza

Klabu ya Nice ya Ufaransa yamsimamisha beki wa Algeria kwa chapisho la utata juu ya Israel-Gaza

Beki wa kimataifa wa Algeria Youcef Atal amesimamishwa kazi na klabu yake ya Nice ya Ligi kuu ya soka Ufaransa baada ya chapisho lake lenye utata kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na mgogoro wa Israel na Palestina.

Ingawa Atal alifuta mara moja chapisho hilo na kuomba msamaha, klabu hiyo imesema kupitia taarifa kwa waandishi wa habari kwamba, kutokana na "uzito" wa maandishi hayo, imechukua hatua za nidhamu mara moja "kabla ya hatua yoyote ambayo inaweza kuchukuliwa na mamlaka ya michezo na kisheria."

Siku ya Jumatatu, waendesha mashtaka wa Ufaransa walianzisha uchunguzi wa awali juu ya Atal kwa tuhuma za "kutukuza ugaidi".

Tawi la Kusini Mashariki la Baraza la Wawakilishi wa taasisi za Kiyahudi za Ufaransa (CRIF) liliwasilisha malalamiko dhidi ya mchezaji huyo Jumanne.

Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Nice ilithibitisha katika taarifa kwamba ilikuwa ikichunguza kesi hiyo chini ya sheria zinazohusu "utukufu wa ugaidi" baada ya kuarifiwa na wanasiasa wa eneo hilo.

Aidha, waendesha mashtaka pia walisema kuwa polisi pia wangetathmini ikiwa chapisho hilo lingekuwa la kuchochea chuki ya kidini au vurugu.

Atal mwenye umri wa miaka 27, aliitwa katika mkutano wa dharura na uongozi wa klabu aliporejea tu kutoka shughuli za timu ya taifa ya Algeria, wakati alipofanya chapisho hilo.

"Tungependa kusisitiza kwamba sifa na umoja WA OGC Nice inategemea tabia ya wafanyakazi wake wote, ambao lazima wawe kulingana na maadili yaliyotetewa na taasisi hiyo," klabu hiyo ilisema, ikiongeza "dhamira yake thabiti ya kuhakikisha kuwa amani inashinda maoni mengine yote."

Tangu Jumamosi, Atal amekuwa akikosolewa sana kwa kuchapisha video kutoka kwa mhubiri wa Palestina kwenye Instagram, akidaiwa kuitisha vurugu dhidi ya Wayahudi.

Maafisa wa soka, wanasiasa, kundi la Wayahudi na Meya wa mji wa Nice, wote wamelaani ujumbe huo, ambao Atal aliufuta pamoja na kuomba msamaha.

Mashirika ya habari hayajaweza kuthibitisha kwa kujitegemea maudhui ya chapisho la awali.

Ufaransa, ambayo ina idadi kubwa ya Wayahudi na Waislamu, iliimarisha usalama baada ya Hamas kuzindua shambulizi kubwa dhidi ya Israeli mnamo Oktoba 7.

Na maafisa waliiweka nchi hiyo katika hali ya tahadhari kubwa kwa mashambulizi yanayoweza kutokea baada ya mwalimu mmoja kuchomwa kisu hadi kufa siku ya Ijumaa na mwanafunzi wa zamani, katika kile ambacho wanasiasa wamesema ni ugaidi.

Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF) halijatoa maoni tangu siku ya Jumapili huku kamati yake ya maadili ikitarajiwa kumchunguza mchezaji huyo.

Akijibu ukosoaji dhidi yake, Atal aliwaambia wafuasi wake wa mtandao wa Instagram kwamba "hataunga mkono ujumbe wa chuki", bila kuelezea kwa nini alichapisha video hiyo awali.

AFP