Mwanasoka wa Algeria Youcef Atal amesimamishwa kucheza mechi 7 kwa ajili ya chapisho lake mtandaoni kuhusiana na mzozo wa Hamas na Israel / Picha: AFP

Beki wa kimataifa wa Algeria Youcef Atal anayeiwakilisha klabu ya Nice ya Ligi Kuu ya soka nchini Ufaransa, amepigwa marufuku ya kucheza mechi saba na Shirikisho la Soka nchini Ufaransa (LFP) kufuatIa chapisho lake kwenye ukurasa wake wa Instagram kuhusiana na mzozo unaoendelea wa Israel na Hamas.

Kamati ya nidhamu ya Shirikisho hilo (LFP) imetekeleza marufuku ya michezo saba ambayo itaanza tarehe 31 Oktoba kufuatia rufaa kutoka Baraza la Maadili la Taifa.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya nyota huyo pia kusimamishwa kazi kwa muda na klabu yake ya Nice kutokana na maandishi yake mtandaoni.

Atal amejikuta katika hali hiyo baada ya kuchapisha video kwenye Instagram mwezi Oktoba ambayo ililaumiwa sana kwa kuwa ya kukera kwa Wayahudi.

Ingawa mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 27 alifuta video hiyo haraka na kuomba msamaha, tayari lilikuwa limeonekana kwenye ukurasa wake.

Atal: Ninaomba msamaha

Atal hata hivyo ameomba msamaha kupitia ukurasa wake wa Instagram, na kusema: "Ninajua kuwa chapisho langu lilishtua watu wengi, na hiyo haikuwa nia yangu, na ninaomba msamaha.

"Nataka kufafanua maoni yangu bila kuzua utata wowote: ninashutumu vikali aina zozote za vurugu, mahali popote ulimwenguni, na ninaunga mkono waathiriwa wote wa vurugu.

"Sitaunga mkono kamwe ujumbe wa chuki. Amani ni maadili ya kibinafsi ambayo ninaamini sana.”

Licha ya kuomba msamaha, ofisi ya mwendesha mashtaka wa jiji la la Ufaransa la Nice ilithibitisha kupitia taarifa yake kwamba ilikuwa ikichunguza kesi hiyo chini ya sheria zinazohusu "kutukuza ugaidi" baada ya kupokea ripoti kutoka wanasiasa wa eneo hilo.

TRT Afrika na mashirika ya habari