Kylian Mbappe alifunga kwenye mechi yake ya mwisho ya nyumbani akiwa mchezaji wa Paris Saint-Germain siku ya Jumapili lakini mabingwa hao wa Ufaransa walipokea kichapo cha kushangaza cha 3-1 dhidi ya Toulouse usiku ambao walitwaa taji la ubingwa wa Ligue 1.
Mbappe alithibitisha katika video iliyotumwa kwenye mtandao wa kijamii siku ya Ijumaa kwamba ataondoka PSG mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu, na hivyo kuhitimisha ushirikiano wa miaka saba na klabu hiyo.
Real Madrid inatarajiwa kuwa lengo lake mchezaji huyo ambaye kuondoka kwake Paris kumekuwa siri ya wazi tangu Februari alipoifahamisha klabu hiyo kwa faragha nia yake ya kuhama.
Mbappe alivaa kitambaa cha unahodha na kufungua ukurasa wa mabao mapema dhidi ya Toulouse na kufikisha jumla ya mabao 44 katika michuano yote msimu huu.
Hata hivyo, Thijs Dallinga aliwasawazishia wageni hao kwa haraka dhidi ya timu ya PSG ambayo ilionyesha mabadiliko 10 kwa timu hiyo iliyotupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Borussia Dortmund katika nusu fainali katikati ya juma, huku Mbappe akiwa ndiye mchezaji pekee aliyehifadhi nafasi yake.
Yann Gboho aliifungia Toulouse kwa bao zuri sana kipindi cha pili, na Frank Magri akamalizia ushindi huo dakika za lala salama huku PSG wakipoteza kwa mara ya pili kichapo cha Ligue 1 msimu huu, na cha kwanza kati ya michezo 27 tangu Septemba.
Mbappe sasa ameifungia PSG mara 256, ikiwa ni rekodi ya klabu, tangu aliposajiliwa kutoka Monaco mwaka 2017 kwa mkataba wa thamani ya euro milioni 180 ($194 milioni).
Idadi yake ya mabao 191 katika ligi kuu ya Ufaransa - ikiwa ni pamoja na 16 akiwa na Monaco mwanzoni mwa maisha yake ya soka - inamweka katika nafasi ya saba kwenye orodha ya wachezaji wa muda wote. Kocha Luis Enrique alimtaja mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 kama "gwiji wa klabu" alipozungumza na vyombo vya habari usiku wa kuamkia mchezo huo.
Mizomo
PSG walikuwa wamebainisha kuwa sherehe baada ya mechi ya Jumapili zingetolewa kwa ajili ya kunyakua taji lao, badala ya kumuenzi Mbappe mwenyewe.
Kulikuwa na hata dhihaka kutoka kwa umati wa mshambuliaji huyo wakati timu zikisomwa kabla ya mchezo, ingawa onyesho kubwa lilifunuliwa kabla ya kuanza kwa upande mmoja wa uwanja ukimuonyesha Mbappe katika pozi la alama yake rasmi huku mikono yake ikiwa imekunjwa.
Klabu hiyo inayomilikiwa na Qatar tayari ilikuwa imemaliza taji la 12 la Ufaransa lililoongeza rekodi, na la 10 katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, kabla ya kuwakaribisha Toulouse ambao wenyewe walikuwa salama kutokana na tishio lolote la kushuka daraja.
Kukatishwa tamaa kwa PSG katika Ligi ya Mabingwa kunamaanisha kwamba Mbappe ataondoka katika klabu hiyo bila kupata zawadi kubwa zaidi ya soka barani Ulaya.
Akiwa na Mbappe, PSG walikuwa washindi wa pili mwaka 2020 na wametinga hatua ya nne bora mara mbili zaidi, lakini nahodha huyo wa Ufaransa sasa ana matumaini ya kutwaa taji hilo katika klabu yake ijayo.
PSG bado wanaweza kumaliza msimu kwa kukamilisha kazi safi ya kufutia mataji ya nyumbani, watakapomenyana na Lyon kwenye fainali ya Kombe la Ufaransa mjini Lyon mnamo Mei 25.
Pamoja na Ligue 1, tayari wameshinda Kombe la Mabingwa, sawa na Kombe la Super Cup la Ufaransa.
Kikosi cha Luis Enrique kitakamilisha kampeni ya ligi kwa kutembelea Nice Jumatano kabla ya kwenda Metz siku ya mwisho ya msimu Jumapili ijayo.