Jamaica, 'Reggae Girlz' ni timu ya kwanza ya Karibea kucheza Kombe la Dunia la Wanawake./ Picha: Reuters

Burudani ya soka kutoka kwa timu ya wanawake ya Jamaica, maarufu 'Reggae Girlz' imekatika baada ya goli la Catalina Usme dakika ya (51') kuipa Kolombia ushindi wa 1-0 kwenye mechi ya Raundi ya 16 ya Kombe la Dunia la Wanawake nchini Australia na New Zealand.

Kabla ya goli la Colombia kwenye raundi ya 16 bora, Jamaica ilimaliza mechi za hatua ya makundi, bila kufungwa hata goli moja kwenye fainali hizi za kimataifa.

Nahodha wa Jamaica Khadijah Shaw, anayeichezea Manchester City, amekuwa tegemeo la timu. Picha:AFP

Hata hivyo, licha ya safari ya Jamaica kufikia tamati, timu hiyo imejishindia nyota za wapenzi wa soka kutokana na ukakamavu wao licha ya changamoto za kifedha, maandalizi duni na hata kutegemea mchango wa fedha za matumizi kupitia mtandao.

Ikiwa unaamini na unafanya kazi kwa bidii chochote kinawezekana. Tumetoka hapa usiku wa leo, tulisimama kwa miguu yetu. Mwisho wa siku tulijua itakuwa ngumu lakini tulifanya kile tulichoweza.

Khadija Shaw, mshambuliaji wa Jamaica

Timu hiyo ilirejesha matumaini yake ya kucheza soka kufuatia juhudi za bintiye mwimbaji Reggae Bob Marly, Cedella Marley, aliyejitolea kuwa balozi rasmi wa timu na kuanzisha kampeni nyingi za kuchangisha pesa kuisaidia timu hiyo.

Kwa karibu muongo mmoja, Cedella Marley amekuwa akigharamia kwa sehemu kubwa mazoezi na usafiri wa Jamaica./ Picha: AFP

Aidha, mbali na Cedella Marley, Sandra Phillips-Brower ambaye ni mama yake kiungo wa timu hiyo Havana Solaun, pia aliendesha mchango wa fedha kupitia ukurasa wa 'Gofund me' na kukusanya zaidi ya dola $76,000 za marekani.

Kabla ya mechi za kombe la dunia, timu hiyo ilifichua kughadhabishwa kwake na maandalizi duni, huku wachezaji wakitoa taarifa iliyosema, "Katika miezi ya hivi karibuni, kwa sababu ya kutopangwa kwa gharama za kambi, tumekosa mechi kadhaa za kirafiki za FIFA.

Hii bila shaka itaathiri maandalizi yetu ya Australia." Mara nyingi, tumekaa na shirikisho ili kueleza kwa heshima matatizo yanayotokana na mipango midogo midogo, usafiri, malazi, masharti ya mafunzo, fidia, mawasiliano, lishe na upatikanaji wa rasilimali zinazofaa.

Baada ya kushinda Mexico, Haiti na Costa Rica na kufuzu kwa Kombe la Dunia la mwaka huu, Jamaica iliendelea kuweka historia kwa kuwaondoa washindi wa zamani wa michuano hiyo Brazil na kumaliza nafasi ya pili katika Kundi F.

Ingawa Jamaica imeliaga Kombe hilo, Kolombia inandelea na safari kumenyana na England baada ya kuweka historia kwa kutinga robo fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake kwa mara ya kwanza kufuatia ushindi wake katika Uga wa Melbourne Rectangular.

TRT Afrika