Gor Mahia ya Kenya kuchuana na Al Ahly, baada ya kuwalaza Mabingwa wa Sudan Kusini. Picha: Gor Mahia

Mchuano mkali unatarajiwa kati ya Gor Mahia ya Kenya, inayolenga kuweka historia kwa kuwa klabu ya kwanza ya Kenya kufikia hatua ya makundi CAF, dhidi ya Ahly ambayo pia inasaka kuwa timu ya kwanza kushinda Ligi ya Mabingwa Mara tatu mfululizo.

Hii ni baada ya Gor Mahia kufuzu kwa duru ya mchujo kwa kuwapiga wageni Al Merreikh Bentiu wa Sudan Kusini 5-1.

Licha ya Al Merreikh Bentiu kutangulia kupitia bao la Samuel Akinbinu aliyezaliwa Djibouti, Gor ilisawazisha baada ya dakika moja tu kupitia Chris Ochieng.

Kufikia muda wa mapumziko, Gor Mahia, ilizidisha uongozi wake kwa kujipa mabao mawili zaidi, kupitia Alpha Onyango na Alphonce Omija.

Baada ya kurejea kutoka mapumziko, Rooney Onyango alizidisha uongozi wa Gor kwa kuongeza mabao mawili na kufikisha jumla ya mabao ya Gor 5-1.

Gor Mahia inaelekea mechi yake dhidi ya mabingwa wa Afrika mara 12 AL Ahly mwezi Septemba ikiwa na matumaini makubwa kunasa angalau Dola za kimarekani 850,000 iwapo itafuzu kwa hatua ya makundi ya timu 16.

TRT Afrika na mashirika ya habari