Biniam Girmay wa Eritrea amekuwa mwendesha baiskeli wa kwanza Mwafrika Mweusi kushinda hatua kwenye Tour de France aliposhinda mbio zilizopunguzwa mwishoni mwa hatua ya tatu Jumatatu.
Girmay, ambaye tayari alikuwa Mwafrika Mweusi wa kwanza kushinda hatua kubwa ya shindano la Italia, Giro d'Italia 2022, aliweza kujipima kasi yake vyema zaidi hadi kuwashinda Fernando Gaviria wa Colombia na Mbelgiji Arnaud de Lie, wa pili na wa tatu mtawalia.
''Sikuwahi kuota ndoto kuwa ningeshiriki Tour de France,'' Girmay aliyejawa na machozi ya furaha alisema. ''Kwa hiyo kupata ushindi kama huu ni kitu kisichoaminika. Namshukuru Mungu sana,'' alisema Girmay baada ya kupata ushindi.
Kwa furaha yake baada ya ushindi, Gimray aliweka picha katika mtandao wa X na maelezo mafupi kabisa, ''Acha nifungue milango'', akielezea kuwa ni wakati wa Waafrika sasa na anatumai wengi zaidi watamfuata.
''Wa Eritrea wote na Waafrika kwa jumla lazima tujivunie kwasababu sasa pia sisi tunatajika katika mashindano makubwa ya kidunia,'' aliongeza Girmay.
Richard Carapaz aliongoza kwa jumla, na kuwa mwendesha baiskeli wa kwanza kutoka Ecuador kuvaa jezi ya manjano, ambayo alimpokonya Tadej Pogacar kwenye nafasi zilizoongezwa bila tofauti za wakati.
Jasper Philipsen wa Ubelgiji ambaye ni kipenzi cha kabla ya jukwaa alihusika katika ajali kubwa ikiwa na umbali wa kilomita 2.3 kutoka kwa jukwaa.
Pogacar, pamoja na bingwa mtetezi Jonas Vingegaard, hawakuathiriwa huku Carapaz akipigana hadi mbele ya peloton kuhakikisha angetwaa jezi ya njano.