Nyota wa DRC Fiston Mayele, ameteuliwa kuwania tuzo ya mwanasoka bora Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi ya nyumbani, barani Afrika. Picha: Mashirika mbalimbali

Shirikisho la soka barani, CAF imezindua orodha ya wagombea watatu watakaowania mwanasoka bora Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi ya nyumbani barani Afrika, Tuzo za Caf 2023.

Mshambuliaji matata, Fistoin Mayele wa timu ya taifa ya DRC na klabu ya Pyramids ya Misri, ametajwa kwenye orodha hiyo ya wachezaji watatu wakiwemo Peter Shalulile (Namibia, na Mamelodi Sundowns) na Percy Tau wa Afrika Kusini na Al Ahly kushindania tuzo hiyo.

Aidha, Mayele ametambulika barani Afrika kwa kujinyakulia kiatu cha dhahabu kwenye Kombe la Shirikisho CAFCC akimaliza msimu kwa kufunga magoli mabao 7.

Shirikisho la soka barani CAF, pia imemtambua Mayele kwa kuichangia klabu ya Yanga kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika CAFCC, kwa mara ya kwanza katika historia yake, 2022/2023.

Wakati huo huo, Mayele pia amejishindia nafasi kwenye nyoyo za mashabiki wa Yanga baada ya kuisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa mataji ya Ligi Kuu, FA Cup na Ngao ya Jamii.

Mayele, mwenye umri wa miaka 29, pia aliibuka mchezaji bora wa Ligi kuu Tanzania bara, NBC Premier League, 2022/23.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga, pia, alitunukiwa mfungaji bora wa Ligi kuu Tanzania bara, NBC Premier League, 2022/23, akiwa na mabao 17.

Wakati huo huo, Mayele alijumuishwa kwenye kikosi bora cha ligi hiyo, msimu wa 2022/23 na pia kutwaa zawadi ya goli bora la msimu.

Mshindi kati ya Mayele, Shalulile na Percy Tau, atajulikana rasmi Jumatatu, tarehe 11 Desemba 2023, kwenye hafla itakayoandaliwa ukumbi wa Palais des Congrès, Movenpick, Marrakech, Morocco.

TRT Afrika