Nyota chipukizi Wilfried Nathan Douala ambaye aliwavutia wengi baada ya kuitwa kikosi cha Kamerun kilichoshiriki Afcon iliyokamilika Ivory Coast, amepatikana na sakata la kudanganya kuhusu "umri wake" na utambulisho mara mbili.
Ingawa hakucheza hata dakika moja wakati wa Afcon ya hivi majuzi kule Ivory Coast, alipata umaarufu kwa kuonekana kuitwa kwenye timu akiwa na umri mdogo.
Kiungo huyo wa klabu ya Victoria United, alinaswa kupitia uchunguzi Shirikisho la Kandanda la Cameroon (Fecafoot).
Mbali na Nathan Douala, wachezaji wengine 7 kutoka timu yake pia wamesimamishwa kushiriki mechi za kuwania ubingwa wa ligi ya kitaifa na shirikisho hilo la soka la Cameroon.
Shirikisho la Kandanda la Cameroon (Fecafoot) limetangaza kupitia vyombo kadhaa vya habari nchini humo, kumfungia Douala na wenzake kushiriki mashindano.
Douala alikuwa ni katika orodha ya wachezaji 62 waliozuiwa kucheza mechi za mchujo za kombe la Mtn Elite One nchini humo.
Si mara ya kwanza Cameroon kukumbwa na sakata la udanganyifu wa umri
Mnamo Januari 2023, shirikisho la soka la Cameroon lililazimika kuwatoa wachezaji 21 kati ya 30 wa timu ya taifa ya wachezaji wasiozidi U17 iliyochaguliwa kwa mashindano ya kufuzu Afcon U-17, baada ya uchunguzi wa MRI ili kubaini umri wao halisi kupitia mifupa kuonyesha walidanganya.