Berhanu Eyassu Wossen achaguliwa Rais wa shirikisho la Ndondi Afrika

Jumla ya nchi 44 zilishiriki kwenye kongamano hilo.

Berhanu amechukua nafasi ya aliyekuwa rais Bertrand Mendouga kutoka Cameroon, ambaye alichaguliwa mnamo 2022 kabla ya kusimamishwa mnamo Agosti 2023 na tume ya maadili ya IBA.

Aidha, Berhanu alisalia kuwa mgombea pekee baada ya kujiondoa kwa wagombea wengine.

Rais huyo mpya wa AFBC Wossen aliahidi kusaka msaada zaidi kwa bara: "Ninaahidi kupata ufadhili zaidi wa kifedha kwa bara letu. Wacha tufikirie juu ya mustakbali wetu wa baadaye kwa pamoja kwa sababu lazima tuungane,” Berhanu alisema.

Awali, Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika mwezi Oktoba mjini Durban, Afrika Kusini.

Hata hivyo, mkutano huo uliahirishwa, na kuhamishiwa hadi Ethiopia, baada ya upinzani wa pamoja wa mataifa thelathini ya Kiafrika kwenye orodha ya wagombea urais wa bodi hiyo ya Kiafrika, iliyothibitishwa mwezi mmoja mapema, na tume ya uteuzi kutoka kitengo cha Uadilifu wa ndondi huru (BIIU).

Rais wa Ndondi duniani, Umar Kremlev alitoa wito wa umoja kwa wajumbe hao. "Tuko Hapa leo kuunganisha Afrika nzima na ninafurahi kuona timu ya umoja. Ili kuchukua biashara yetu kwa ngazi inayofuata, tunahitaji matukio zaidi ambapo wanariadha wanaweza kuwa na fursa ya kushinda pesa. Ninaona nchi nyingi barani Afrika ambazo zinahitaji msaada wetu na tumekuwa tukiunga mkono sana.”

TRT Afrika