Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza Desemba 15 kuwa sikukuu ya mapumziko kusheherekea ushindi wa timu ya Taifa ya Raga ya Afrika Kusini baada ya timu hiyo kushinda katika michuano ya Kombe la Dunia la Raga mwishoni mwa juma.
Hii ni mara ya nne kwa Afrika Kusini kushinda kombe hilo na kuweka rekodi mara mbili mfulululizo, mnamo Jumamosi kufuatia ushindi wa 12-11 dhidi ya mahasimu All Blacks ya New Zealand nchini Ufaransa.
"Ili kusherehekea mafanikio makubwa ya timu yetu ya raga, Springboks na mafanikio ya michezo yetu mengine yote wanaume na wanawake - na kama kumbukumbu kwa azimio la umoja wa taifa letu - ninatangaza Ijumaa, tarehe 15 Desemba 2023 kama siku ya mapumziko," rais Ramaphosa aliandika kwenye mtandao wa X.
Ameongeza kuwa siku hiyo pia itakuwa ni sherehe kwa ajili ya timu nyingine za taifa za michezo zilizofanikiwa pia.
"Tunatangaza siku hii kuwa siku ya matumaini, siku ya sherehe na umoja. Wanamichezo wetu wa kiume na wa kike wametuonyesha kinachowezekana. Tutafaulu na tutahakikisha hatumuachi mtu nyuma,” alisema Ramaphosa.
Ramaphosa alisema kuwa hangeweza kutangaza likizo hiyo kwa sasa ili kuruhusu zaidi ya wanafunzi 720,000 wanaofanya mtihani wao wa mwisho mwaka huu, kuhitimisha mitihani yao.