Utekelezaji badala ya maneno tu ndiyo tiba pekee ya maendeleo Afrika

Utekelezaji badala ya maneno tu ndiyo tiba pekee ya maendeleo Afrika

Maneno matupu sio mwarobaini wa changamoto za maendeleo barani afrika
Afrika Kusini ingawa inaongoza kwa uchumi katika bara hilo, inakabiliwa na tatizo la umeme/ Picha: AFP

Na Peter Nyanje

Afrika ina rasilimali watu na rasilimali nyingi ambazo zinapaswa kutumika ipasavyo ili kupata maendeleo upesi.

Zaidi ya nusu karne baada ya nchi zake nyingi kukombolewa kisiasa, Afrika bado inajitahidi kutekeleza wajibu wake kufikia viwango vya maendeleo ya kimataifa licha ya kutajwa kuwa bara lenye fursa kubwa za maendeleo ya kiuchumi.

Mambo kadhaa yanatajwa kuchangia hali hii ikiwa ni pamoja na uongozi mbovu.

Afrika ni bara la pili kwa idadi ya watu na lina ardhi kubwa yenye rutuba kwa kilimo - pamoja na rasilimali kama vile maji, misitu na madini. Viungo hivi ni muhimu katika kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi husika.

Lakini Afrika bado inadorora chini ya kiwango cha maendeleo duniani kote. Ili nchi yoyote ifaidike ipasavyo na rasilimali watu na rasilimali za asili, viongozi wake lazima watoe mwelekeo unaohitajika na kuchukua maamuzi sahihi. Labda jambo hili ndiyo linalokosekana Afrika.

Nchi za Kiafrika pia zina uwezo mkubwa wa nishati ya jua. Picha: Reuters

Ubora wa viongozi pia ni muhimu katika kuanzisha michakato na mafanikio ya kidemokrasia. Mapungufu ya uongozi yanakinzana na hatua za kukua kiuchumi.

Chukua, kwa mfano, mzozo wa sasa wa umeme nchini Afrika Kusini. Tatizo lingeweza kufikia kiwango cha sasa cha mgao wa umeme kama Ethiopia ingeharakisha mchakato wa ujenzi wa bwawa kubwa la kuzalisha umeme kando ya Mto Nile.

Hii ni kwa sababu Ethiopia ingekuwa inazalisha umeme wa ziada ambazo ungeweza kuuzwa kwa Afrika Kusini yenye ukata mkubwa wa nguvu kupitia gridi ya Afrika mashariki.

Ikumbukwe kwamba Tanzania tayari imeunganisha gridi yake na Kenya ambayo imeunganishwa na Ethiopia.

Kwa hiyo, umeme kutoka Grand Ethiopian Renaissance Dam, GERD, ungeweza kufika Afrika Kusini kupitia Kenya, Tanzania na Zambia.

Vilevile, tatizo hili linaloikabili Afrika Kusini leo lisingekuwa changamoto kubwa iwapo viongozi wa Tanzania wasingeachana na mpango wa ‘Uchumi wa Gesi’ uliozungumzwa wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais Jakaya Kikwete.

Kikwete aliingia madarakani mwaka 2005 huku kukiwa na ukame mkubwa ambao uliharibu mabwawa ya kuzalisha umeme ambayo yalikuwa yakizalisha zaidi ya asilimia 70 ya umeme kwa Tanzania.

Ndipo aliamua kufikiria ‘nje ya boksi’ na akaja na mipango ya kutumia rasilimali nyingi ya gesi asilia kusini mwa Tanzania kama chanzo kikuu cha nishati.

Hii ilikusudiwa kuibadilisha Tanzania kutoka katika kutegemea umeme wa maji na kuwa uchumi unaotumia gesi.

Iwapo mpango huo ungetekelezwa, Tanzania leo hii ingekuwa inajitengenezea umeme wa kutosha ikiwa na ziada nyingi ambayo inaweza kuuzwa kwa nchi nyingine zenye uhitaji kama vile Afrika Kusini.

Lakini mipango ya kukuza uchumi wa gesi nchini Tanzania ni sawa na kusema imekufa.

Maumivu ya Kujitakia

Kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC na dada yake wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wangetekeleza wazo lao la kuunganisha mabwawa yao ya umeme, Afrika Kusini ingefaidika na umeme wa Ethiopia.

Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance ni mradi kabambe wa kuongeza uzalishaji wa umeme. Picha: AFP

Hata kama Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance, GERD, lingekwama, Tanzania ingesukuma mpango wa uchumi wa gesi, hadi sasa ingekuwa inazalisha umeme wa kutosha kutokana na rasilimali yake kubwa ya gesi na ikiwezekana kuuza nchi nyingine.

Miezi miwili tu iliyopita, Tanzania ilikuwa katika tatizo la umeme kutokana na uhaba wa mifumo ya uzalishaji.

Hii isingetokea hivyo kama Serikali ingeendelea na mpango wa gesi kama chanzo kikuu cha nishati.

Serikali ya Kikwete ilikuwa imekopa fedha kwa ajili ya kufadhili mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ili rasilimali hiyo ipatikane kwa urahisi kwa matumizi ya viwandani na mengineyo.

Mradi huo uligharimu nchi takriban dola bilioni 1.22. Hata hivyo, serikali iliyofuata iliamua kuachana na mpango wa uchumi wa gesi na kuamua kujenga Bwawa la Umeme la Julius Nyerere kando ya Mto Rufiji licha ya wasiwasi wa wanamazingira na wachumi.

Mpango wa uchumi wa gesi ulikusudiwa kuruhusu Tanzania kutumia gesi kusaidia maendeleo yake ya kijamii na kiuchumi.

Kulikuwa na mipango ya kubadilisha gesi kuwa nishati ya msingi ya kupikia nchini Tanzania, hivyo kuokoa misitu ya nchi ambayo inaharibiwa na watengenezaji wa mkaa. Lakini mipango yote hiyo ilisitishwa.

Pia kulikuwa na mipango ya miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi kwa awamu, ikilenga kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkuu wa kanda.

Miradi iliyopangwa kufadhiliwa zaidi kupitia uwekezaji wa sekta ya kibinafsi na uwekezaji mdogo wa kifedha wa serikali, ilikusudiwa kuzalisha zaidi ya megawati 10,000 baada ya kukamilika.

Lakini miradi yote iliyopangwa na serikali ya Kikwete kuongeza uzalishaji wa umeme ilisitishwa na warithi wake.

Kutokana na hali hiyo, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokumbwa na uhaba wa umeme licha ya kuwa na rasilimali zote zinazohitajika kuzalisha nishati zaidi ya kutosha kwa uchumi wake.

Hivi tunavyozungumza, Tanzania inazalisha umeme chini ya megawati 1,300 kwa wakazi wake zaidi ya milioni 65.

Miaka michache iliyopita, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG, ilieleza katika ripoti yake ya mwaka kuwa deni la mradi wa bomba lililotelekezwa lililowekwa chini ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, TPDC, limelifanya shirika la umma kujiendesha likiwa na mtaji hasi na hivyo kuathiri ukwasi wake.

Kukuza biashara huria

Rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa, alikuwa mtetezi wa biashara ya ndani ya Afrika. Alisisitiza biashara kati ya nchi za Afrika akibainisha kuwa ubadilishanaji huo utakuza uchumi wa nchi hizo na kwamba kwa kufanya hivyo watanufaika zaidi ikilinganishwa na utaratibu wa sasa wa kuuza malighafi zao hasa kwa mataifa yaliyoendelea.

Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance ni mradi kabambe wa kuongeza uzalishaji wa umeme. Picha: AFP

Alitoa hoja hizo akipinga mtazamo wa nchi za Afrika zinazoshinikiza kusaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) na Umoja wa Ulaya (EU). Mkapa aliridhika kwa kiasi fulani wakati bara hilo lilipoamua kuanzisha Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika, AfCTA, likiwa na jukumu la jumla la kuunda soko moja linaloleta pamoja nchi 55 na makundi nane ya kiuchumi ya kikanda yenye jumla ya watu bilioni 1.3 na Pato la Taifa la takriban dola 3.4 trilioni.

AfCTA, ambayo ilianza kutumika Mei 2019, ilidhaniwa kuwa dawa ya matatizo ya biashara ya ndani ya Afrika. Hata hivyo, licha ya kuwa na mataifa 54 kati ya 55 yaliyotia saini mkataba huo kufikia mwezi huu, biashara kati ya nchi za Afrika imeendelea kuwa chini kiasi cha kusikitisha.

Kulingana na takwimu zilizochapishwa Januari 2023 na Africa Renewal, jarida la kidijitali la Umoja wa Mataifa linaloangazia maeneo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa barani Afrika, biashara ya ndani ya Afrika inachangia asilimia 14.4 tu ya jumla ya mauzo ya nje ya Afrika.

Wachambuzi wanatetea kuwa AfCTA inaweza kuwa chombo bora cha kupeleka mbele biashara ya Afrika, lakini kuwa nayo ni jambo moja na dhamira ya kisiasa, ambayo inahitajika kufanya biashara ifanyike kati na miongoni mwa nchi za Afrika, ni jambo tofauti kabisa.

Hivyo ni vigumu kuiona Rwanda ambayo imeanza kutengeneza magari yanayotumia umeme, ikitegemea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwa chanzo cha malighafi ya uzalishaji wa betri kwa sababu miamba hio miwili haipatani licha ya faida ambayo wangepata kwa kuwa nchi majirani.

Kugawana faida

Kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya wote ni chaguo bora kwa nchi za Afrika. Kwa mfano, badala ya ushindani mkali juu ya matumizi ya maji ya Nile, Ethiopia na Misri zingeangalia Shirika la Maendeleo ya Mto Senegal, OMVS, kama kielelezo na chombo muhimu cha kutatua kutoelewana kwao.

Nchi za Kiafrika bado zinapambana kuinua uchumi licha ya rasilimali nyingi. Picha: Reuters

Ilianzishwa mwaka wa 1972, OMVS imeonekana kuwa mfano mzuri zaidi wa usimamizi wa pamoja wa mito, kwani tangu wakati huo, Guinea, Mali, Senegal na Mauritania hazijawahi kugombana kuhusu maji ya Mto Senegal.

Nchi za Kiafrika pia zinapaswa kuzingatia AfCTA kama suluhisho la matatizo yao ya kiuchumi. Juhudi za kila serikali ya Afrika za kuboresha uwiano wake wa kibiashaŕa na dunia zielekezwe katika kuongeza uwiano wa kibiashara na nchi za ndugu za kiafrika.

Hii inaweza kuona nchi za Kiafrika zikigawana utajiri wao na kuunda fursa za ajira kupitia uwekezaji unaowezeshwa na biashara ya ndani ya Afrika.

Biashara inaweza kufanywa kwa urahisi kati ya nchi za Kiafrika kwa kuunganisha vituo vya kiuchumi.

Kwa mfano, EAC imeunganisha Tanzania kwa urahisi na Bahari ya Atlantiki kupitia DRC, ambayo hivi karibuni iliongezwa kuwa mwanachama mpya zaidi wa Jumuiya hio.

Kabla ya hapo, SADC ilikuwa ya kwanza kuunganisha ukanda wa Kalahari kati ya Walvis Bay nchini Namibia na Pretoria nchini Afrika Kusini mwaka 1998 kabla ya kupanuliwa hadi Maputo, Msumbiji, hivyo kuunganisha Bahari ya Atlantiki na Bahari ya Hindi.

Mwandishi, Peter Nyanje, ni mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi aliyeko Dar es Salaam, Tanzania.

Angalizo: Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayawakilishi msimamo, maoni na sera za uhariri za TRT Afrika.

TRT Afrika