Na Shamsiyya Ibrahim
Muswada wa kihistoria ulioletwa katika bunge la Nigeria, unapendekeza adhabu ya kifungo cha miaka 10 jela kwa wanaoongoza shughuli za kitapeli za Upatu na hivyo kuufanya muswada huo uonekeane kama kinga inayohitajika sana dhidi ya udanganyifu kwa mamilioni ya wawekezaji walionaswa kati ya ahadi ya faida kubwa na uwongo wa waendeshaji wanaofanya shughuli hio kwa siri.
Hatua hiyo imekuja baada ya maumivu ya muda mrefu ya mamilioni ya Wanigeria ambao tayari wameangukia kwenye hadaa iliyokula akiba waliyojikusanyia maisha yao yote.
Hadi kufikia mwaka 2022, Wanigeria walikuwa wamepoteza zaidi ya naira bilioni 300 kwa miradi ya Upatu haramu. Hayo yalifanyika katika kipindi cha miaka mitano pekee, kulingana na ripoti inayoangazia Uwekezaji wa Fedha ya Norrenberger.
Rais wa Seneti, Ahmad Lawan anasema mswada huo unakusudiwa kuwalinda wawekezaji kwa kudhibiti vilivyo soko na kupunguza hatari za kimfumo, mbali na kuweka adhabu kali zaidi kwa wasimamizi wa shughuli za upatu haramu.
Hassan Sardauna Yamayo, mchambuzi wa masuala ya kijamii na mtaalamu wa sera za fedha, anaamini kuwa mswada huo umekuja wakati sahihi.
"Ni uamuzi muhimu sana katika historia ya Nigeria. Shughuli za utapeli zinazidi kuwa za kawaida katika sekta zote, iwe Yahoo-Yahoo, wadukuzi, walaghai au waendelezaji wa upatu haramu. Yote haya yalihitaji kushughulikiwa kwa nguvu," alisema.
Yunusa Abubakar, mbunge wa bunge dogo, anasema mswada huo ulitarajiwa kusaidia utendakazi wa soko la mitaji na kuwezesha sekta mbalimbali za kiuchumi nchini humo.
"Lengo ni kufanya aina hii ya biashara isiyoeleweka kuwa jambo gumu huko tuendako" anaiambia TRT Afrika.
Tatizo Sugu
Ingawa kupitishwa kwa muswada huo bungeni kulifanyika bila matatizo, bado unasubiri saini ya rais ili kuwa sheria.
"Nimefurahishwa sana na hatua hii iliyochukuliwa na Bunge. Natumaini utatiwa saini kuwa sheria haraka iwezekanavyo," anasema Fauziyya Hussaini, mhanga wa utapeli wa upatu.
Mbunge Abubakar anaona muswada huo ukirejesha imani ya Wanigeria milioni 150 kwa Utawala baada ya kuonyesha azma na uwezo wa kulinda maslahi yao.
Kulingana na Tume ya Usalama na Ubadilishanaji wa Fedha ya Nigeria, Wanigeria milioni tatu kwa jumla walipoteza naira bilioni 18 pale Upato unaojulikana kama MMM (Mavrodi Mundial Movement) uliposambaratika mwaka 2016.
Kiwango cha upotevu wa fedha hakikuwazuia waendeshaji wa Upatu kufikiria njia mpya za kutapeli watu au wawekezaji kuweka pesa zao katika miradi hii.
Janga la udanganyifu Miradi ya Upatu kwa ujumla hutumia mkakati wa uuzaji wa piramidi, kuunda biashara hewa ambayo huwavutia watu kwa ahadi ya mapato ya juu kwenye uwekezaji baada ya muda maalum.
Mtaalamu wa usalama wa mtandao, Yusufdeen A Yusuf anataja kuenea kwa biashara hizo za piramidi nchini Nigeria "inatisha na inatia wasiwasi", zaidi kwa sababu tamaa ya pesa rahisi haipungui licha ya kuwa mitego inajulikana.
Zainab Shehu ni mmoja kati ya Wanigeria wengi walioweka pesa zake alizozichuma kwa taabu katika upatu ulioonyesha ahadi kedekede. Alipoteza takriban naira 700,000 baada ya kutambulishwa kwa biashara ya mtandaoni na rafiki yake. Uzoefu huo ulimwacha Zainab akiwa amechanganyikiwa kabisa.
Sheria mpya iliyopendekezwa ya kuzuia matukio kama haya kutokea mara kwa mara ni jambo ambalo anatumaini litafanya uwekezaji kuwa na hatari ndogo kuliko wakati alichoma mfuko wake. "Ninakaribisha uamuzi huu wa Bunge la Kitaifa kwani utakuwa onyo kali kwa walaghai," anasema.
Mwekezaji mwenzake, Fauziyya, ambaye alipoteza zaidi ya naira 500,000 katika miradi miwili ya Upatu, alikumbuka kuwa uzoefu mbaya zaidi ulikuwa maumivu ya kiakili aliyopitia.
"Sitawahi kumshauri mtu yeyote kuweka pesa zake katika uwekezaji kama huo. Kutafuta pesa rahisi kamwe hakuleti matokeo chanya,” anaonya.
Hatua inayofuata kwa sheria inayopendekezwa ni kupitia mchakato wa kile Abubakar anachokielezea kama "kuupiga msasa muswada" kabla ya kupelekwa kwa Rais, ambaye ana siku 30 za kutia saini ili kuwa sheria nchini.
Kusafisha mfumo
Iwapo Rais atakataa au kugoma kutia saini muswada huo, anapaswa kulitolea bunge sababu za msingi za kutofanya hivyo.
"Ikiwa tutakubaliana na hoja zake, basi tunaweza kurekebisha mswada huo, na ikiwa hatutafanya au anakataa kutoa mrejesho baada ya siku 30, Bunge la Kitaifa lina kila haki ya kukiuka wajibu huo wa Rais," Abubakar anafafanua.
Kauli ya mbunge huyo inaleta matumaini kwa waathiriwa kama Fauziyya na Zainab, ambao wamekuwa wakisubiri kwa hamu kuona matapeli hao wakipelekwa jela.
"Shughuli za watu kama hao zina athari mbaya kwa watu na uchumi. Nina matumaini kuwa muswada huu hakika utaleta mabadiliko, hata kama ni kidogo, hasa wakati huu ambapo shughuli za Upatu zinashamiri zaidi kuliko hapo awali," anasema mchambuzi mambo ya kijamii, Yamayo.
Akilipongeza bunge kwa kuchukua hatua kubwa za awali, anawataka wabunge kuhakikisha kanuni ya kutoa hukumu kwa wadanganyifu inatumika kwa kila mtu, bila kujali hali ya kijamii au kisiasa.
Mtaalamu wa masuala ya usalama wa mtandao, Yusuf, pia ana imani kuwa muswada huo utawaweka waendeshaji wa Upatu nchini Nigeria kitanzini. Anapendekeza kwamba mamlaka sasa inapaswa kuzingatia kuongeza uelewa miongoni mwa Wanigeria kuhusu hatari za kutafuta pesa za haraka-haraka.
"Kama Wanigeria wanaweza kuwekwa mbali na vishawishi na udanganyifu wa matapeli, hilo lenyewe litasaidia sana kuzuia tishio la Upatu," anaiambia TRT Afrika.