Somalia yajiunga na kambi ya biashara ya Afrika Mashariki katika 'hatua kubwa'. Picha: Ikulu ya Somalia

Uanachama wa Somalia ulitangazwa rasmi katika mkutano wa kilele wa EAC katika mji wa Arusha, Tanzania huku ikijiunga na Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.

Jumla ya mapato ya biashara ya Jumuiya ya EAC imetajwa kuwa billion 78.75 mnamo 2022.

Rais Hassan Sheikh Mohamud alitaja tangazo la siku ya Ijumaa kama "sura mpya" katika historia ya Somalia, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikisumbuliwa na migogoro, machafuko ya kisiasa na majanga ya hali ya hewa.

Somalia inasifika kwa kujivunia ukanda mrefu zaidi wa pwani bara la Afrika huku ikiwa na zaidi ya kilomita 3,000 (maili 1,800) na uanachama wake ni mlango wa EAC uarabuni.

Ni wanachama wengine wawili pekee - Kenya na Tanzania wenye bahari.

Hata hivyo, wachambuzi wamesema kuwa, ingawa uanachama wa Somalia utapiga jeki Jumuiya ya Afrika Mashariki kiuchumi, bado kuna changamoto za kiusalama huku taifa hilo likiendelea na juhudi za kukabiliana na makundi ya kigaidi.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia uliandika kwenye mtandao wa X, iliyokuwa Twitter, kuwa ilikuwa "hatua nyingine muhimu katika kurejea kwa Somalia katika nafasi yake kwenye jamii ya kimataifa na ushiriki na majirani zake."

Aidha, nayo ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) pia uliisifu ujumuishaji wa Somalia kama "historia" na hatua mpya kuelekea ushirikiano wa kikanda na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

AFP