Benki Kuu ya Rwanda imeonya dhidi ya kupanga bei za bidhaa na huduma katika sarafu za kigeni kutokana na ripoti za ndani kuhusu kudorora kwa sarafu ya ndani dhidi ya dola ya Marekani.
Katika taarifa siku ya Jumamosi, gavana wa benki kuu alisema kwamba shughuli zote nchini zinapaswa kulipwa kwa sarafu ya Rwanda, kama inavyotakiwa na sheria au kukubaliwa na wahusika.
Taarifa hii inakuja wakati sarafu ya ndani inaposhuka thamani kwa zaidi ya asilimia 8, ambayo imesababisha kupungua kwa thamani.
"Mtu yeyote anayeuza au kupanga bei za bidhaa au huduma katika sarafu ya kigeni bila idhini atakuwa anastahili adhabu ya kukamatwa na kutaifishwa kwa kiasi kinachohusika katika shughuli hiyo," alisema gavana wa benki, John Rwangombwa, akirejelea vipengele vya sheria.
Ukuaji wa uchumi wa Rwanda umepungua mwaka huu hadi asilimia 6.2 baada ya kurekodi ukuaji wa asilimia 8.2 mnamo 2022, waziri wa fedha na gavana wa benki kuu walisema mwezi uliopita.
Ukuaji unatarajiwa kupanda hadi takriban asilimia 7.5 mnamo 2024 na 2025.
Kumekuwa na wasiwasi kuhusu uhaba wa dola ya Marekani nchini, pamoja na kudorora kwa sarafu ya ndani, tovuti ya New Times ya nchini humo inaripoti.
Nchi hii ya Afrika Mashariki ilikuwa miongoni mwa uchumi unaokua kwa kasi zaidi kwenye bara hilo kabla ya kuanza kwa janga la Uviko-19 kama inavyopimwa na pato la taifa lake.