Kufuatia ombi la Baraza la Biashara la Afrika Mashariki la kuongeza ushuru unaolipwa kwa nguo zinazoagizwa kutoka nje kwa bei ya juu zaidi, wafanyabiashara ya nguo Afrika Mashariki wanakaribia kukutana na kigingi kipya.
Kutokana na mapendekezo ambayo yametolewa katika mkutano mkuu wa 38 wa baraza hilo uliofanyika mkoani Kilimanjaro, nchini Tanzania.
Kulingana na baraza hilo ambalo ni chombo muhimu kwa biashara na uwekezaji katika eneo hilo, ushuru wa pamoja kwenye uingizajia wa nguo unapaswa kuongezwa kutoka 25% hadi 35%, kiwango cha juu zaidi cha ushuru chini ya EAC.
Hatua hii inalenga kuhimiza uzalishaji wa ndani wa pamba katika ukanda wa Afrika mashariki kwani uagizaji wa zao la pamba kutoka mataifa ya nje kihistoria umekuwa ukikwamisha ukuaji wa sekta hiyo.
Tangu Januari 1, 2005, bidhaa zilizoingizwa katika ukanda huu zilitozwa ada ya ushuru ya 25%, huku mali ghafi zikiwa hazitozwi ushuru wowote.
Biashara ya mavazi inachangia pakubwa katika uchumi wa jumla wa EAC. Kenya, kwa mfano ni mwagizaji mkubwa zaidi katika jumuiya ya Afrika Mashariki, wa pamba kutoka nchi za nje.
Viongozi wa nchi hizo pia wanataka kuunda mfumo wa kidijitali ili kuwezesha ubadilishanaji wa data kuhusu uvunaji wa pamba na biashara ya pamba. Haya yote yanafanywa ili kukuza biashara kati yao.
Mkutano huo umezitaka nchi shirika kutumia vazi la asili kama vazi la serikali kwa sherehe za umma kama sehemu ya uhamasishaji wa Kununua bidhaa kwa `kauli mbiu Nunua Afrika Mashariki,Jenga Afrika Mashariki(BEABEA-Buy East Africa,Build East Africa).
Kama mkakati wa kusaidia biashara ya nguo, Kenya hapo awali iliwahimiza wafanyikazi wa umma kuvaa mavazi ya Kiafrika siku ya Ijumaa, na wafanyikazi wa umma wanakumbatia utaratibu huo polepole.
Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta alifufua upya kiwanda cha nguo Kenya Rivatex mwaka wa 2020 ili kuhimiza utengenezaji wa bidhaa zinazotengenezwa katika taifa hilo kwa kutumia pamba inayokuzwa nchini humo.
Kuanzia miaka ya 1980, uzalishaji wa pamba ulikua umepungua kwa kiasi kikubwa, na Kenya imelazimika kutegemea bidhaa kutoka nje.
Mataifa shirika yanatarajia kuwa msimamo huu mpya utaongeza uzalishaji katika ukanda wote wa Afrika Mashariki.