Rais wa DRC Felix Tshisekedi aliongoza ufunguzi wa Kituo cha Kifedha cha Kinshasa mnamo Desemba 19, 2023. / Picha: TRT Afrika

Katika juhudi za kukuza uchumi wa nchi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imezindua kituo kikuu cha fedha katika mji mkuu wa Kinshasa.

Kituo cha Fedha cha Kinshasa kipo katika eneo la kimkakati la Gombe, magharibi mwa DRC.

Ujenzi wa majengo 11 katika eneo la mita za mraba 165,000 ulianza mwezi Februari 2022, na kukamilika mwezi Desemba 2023.

Ubunifu na ujenzi wa jengo la kisasa umefanywa na kampuni ya ujenzi ya Kituruki Milvest, tawi la Miller Holding.

Kituo kikuu cha kifedha kilijengwa kwa gharama ya $ 290 milioni. / Picha: TRT Afrika

Kituo kina nini?

Kituo kina taasisi muhimu kama vile Wizara ya Fedha na Bajeti, Mkurugenzi Mkuu, Mkaguzi Mkuu, Sekretarieti Kuu ya Fedha na Benki ya Maendeleo. Kuna taasisi tisa zinazohusiana na wizara ya fedha.

Kituo kinasimamiwa na shirika la biashara la Investment Fund linalomilikiwa na serikali, ambalo linasimamia mali isiyohamishika.

Jengo la ofisi za kitaalamu lenye ghorofa 19 ndilo refu zaidi. Ndani ya eneo hilo, kuna muunganiko wa hoteli, uwekezaji binafsi wa kampuni ya Milvest.

Miongoni mwa sifa za kipekee za kituo cha fedha ni kituo chake cha kisasa cha mikutano chenye uwezo wa watu 3,000, kikifanya kuwa moja ya vituo vikubwa vya mikutano barani Afrika.

Mahusiano ya Uturuki na DRC

Kuna pia ukumbi maalumu kwa mikutano midogo ambayo kwa ujumla inaweza kuchukua hadi watu 10,000.

Kwa wageni wa biashara, kituo kina hoteli yenye vyumba 240 na eneo la maegesho ya magari 1,100.

Mwezi Februari 2022, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitembelea DRC kama sehemu ya uhusiano wa pande mbili kati ya Uturuki-DRC.

Wakati wa ziara yake, Erdogan alisaini mikataba kadhaa ya usalama, ulinzi na miundombinu.

Kituo cha Kifedha cha Kinshasa ndicho kituo kikubwa zaidi cha kibiashara nchini DRC. / Picha: TRT Afrika

Makubaliano

Kulingana na masharti ya mkataba wa ujenzi, miundombinu ya kiwango cha juu iliyojengwa na Milvest itakuwa mali ya serikali ya DRC baada ya miaka 49.

Mwenyekiti wa Miller Holding, Turhan Mildon, aliambia TRT Afrika kwamba masuala ya kimkakati yalikuwa changamoto kubwa wakati wa ujenzi.

Zaidi ya watu 1,500 walihudhuria sherehe ya ufunguzi tarehe 19 Desemba. Raia wa Congo wamepokea kwa mikono miwili mradi huo uliojengwa kwa gharama ya dola milioni 290.

Uzinduzi rasmi ulifanyika masaa machache kabla ya uchaguzi mkuu wa DRC tarehe 20 Desemba, 2023.

TRT Afrika