Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma alisema chama chake kipya kitajiunga na muungano wa upinzani ili kuratibu upinzani dhidi ya serikali, huku kikidumisha pingamizi kwa matokeo ya uchaguzi mkuu.
MK ilisema itajiunga na kikundi kipya cha wabunge ambacho kinajumuisha vyama vingi vya upinzani vyenye mrengo wa kushoto vinavyowakilishwa bungeni.
Muungano huo w aupinzani unaojiita "Progressive Caucus" kwa sasa unaongozwa na chama chenye siasa kali za mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters (EFF), ambacho kilishinda viti 39 katika bunge jipya.
Licha ya "wizi wa mchana" wa kura, vyama vinavyounda muungano huu vilipata takriban "asilimia 30 katika bunge la kitaifa," alisema msemaji wa chama cha uMkhonto weSizwe (MK) Nhlamulo Ndhlela.
Hilo, alisema, "linatuweka katika nafasi nzuri sana ya kupigania ukombozi kamili wa kiuchumi wa watu weusi na Waafrika".
Ndhlela alikuwa akisoma taarifa kwa niaba ya rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 82. Zuma, alikaa kimya huku hotuba yake ikisomwa, mara kwa mara akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari.
"Uchaguzi wa 2024 uliibiwa" alisema Ndhlela. "Tumeiagiza timu yetu ya kisheria kuchukua hatua zozote zinazowezekana ndani ya Afrika Kusini na kimataifa ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka".
Na akaongeza: "Kwa wakati ufaao tutawaita watu wetu kudhihirisha kutoridhika kwao dhidi ya dhuluma hizi zote kwa amani, mitaani, mahakamani na hata bungeni hadi pale malalamiko yetu yatakapopatiwa ufumbuzi."
Chama cha MK kilishika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo, kwa kujinyakulia asilimia 14.6 ya kura na viti 58 vya ubunge.
'Muungano usio mtakatifu'
Siku ya Ijumaa, chama hicho kilisusia kikao cha kwanza cha bunge la nchi hiyo ambapo hasimu wa muda mrefu wa Zuma wa kisiasa Cyril Ramaphosa alichaguliwa tena kuwa rais kwa muhula wa pili.
Ingawa chama hicho kilisema wabunge wake sasa watakuwepo katika Bunge la Kitaifa, pia kilitangaza kuwa kimezindua ombi jipya la mahakama kupinga matokeo "yaliyoibiwa" ya uchaguzi.
Tayari ilikuwa imeenda kortini kujaribu kuzuia bunge jipya kuitishwa, na iliwasilisha malalamishi tofauti kuhusu madai ya ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
Vyama vingine kadhaa pia vimelalamikia baraza la uchaguzi nchini humo na kuwasilisha malalamishi ya kisheria.
Ramaphosa, ambaye ataapishwa mnamo Juni 19, ataongoza kile anachokiita serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi wa Mei kutotoa mshindi wa moja kwa moja.