Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma anatarajiwa kufika katika Mahakama Kuu ya Gauteng mjini Johannesburg siku ya Alhamisi kuendelea na kesi yake dhidi ya Rais Cyril Ramaphosa.
Zuma anamtuhumu Ramaphosa kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya mwendesha mashtaka wa Afrika Kusini Billy Downer (SC) na mwandishi wa habari Karyn Maughan, ambao kwa pamoja, wanadaiwa kuanika taarifa zake za matibabu katika kesi dhidi ya ufisadi, mwaka 2021.
Zuma alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi 15 jela mwaka huo huo kwa kukaidi agizo la mahakama la kufika mbele ya tume ya mahakama inayochunguza tuhuma za ufisadi katika serikali na makampuni yanayomilikiwa na serikali wakati wa muhula wake wa urais kuanzia 2009 hadi 2018.
Zuma anadai kuwa kufichuliwa kwa rekodi zake za matibabu kulikiuka Sheria ya Mamlaka ya Mashtaka ya Kitaifa (NPAA). Kesi hii ilisikilizwa kwa mara ya mwisho mahakamani Disemba 2023.
Maombi yaliyoshindikana
Mwaka 2023, Ramaphosa alifanikiwa kutuma maombi kwa mahakama ya kukagua na kutengua ombi la kibinafsi la Zuma. Zuma alitaka kukata rufaa dhidi ya uamuzi huu mbele ya jopo la Mahakama Kuu, lakini akashindwa.
Pasipo kuchoka, Zuma aliwasilisha ombi kwa Mahakama ya Juu ya Rufaa, lakini mahakama ya rufaa ilitupilia mbali rufaa yake. Tangu wakati huo ameiomba Mahakama ya Rufaa iangalie upya uamuzi wake.
Siku ya Jumanne, Mahakama ya Uchaguzi ya Afrika Kusini iliamua kwamba Rais wa zamani Jacob Zuma anaweza kugombea wadhifa wa mbunge katika uchaguzi ujao, na kubatilisha uamuzi wa awali ambao ulikuwa umemzuia kugombea uchaguzi huo.
Uamuzi huo unafungua njia kwa Zuma kugombea urais kupitia chama cha Umkhonto weSizwe, chama kipya cha kisiasa ambacho alijiunga nacho mwaka jana baada ya kukilaani chama tawala cha African National Congress (ANC) ambacho aliwahi kukiongoza.
Tume Huru ya Uchaguzi hapo awali ilitoa uamuzi kwamba Zuma hakuwa na sifa ya kugombea nafasi hiyo kutokana na rekodi yake ya uhalifu baada ya kupokea pingamizi dhidi ya kugombea kwake.