Zimbabwe yamwita balozi wa Marekani huku kukiwa na madai ya kuingilia uchaguzi

Zimbabwe yamwita balozi wa Marekani huku kukiwa na madai ya kuingilia uchaguzi

Machapisho ya mitandao ya kijamii ya ubalozi wa Marekani yameelezwa kuwa yanaingilia masuala ya ndani ya Zimbabwe
Ubalozi wa Marekani unashutumiwa kwa "kuwafundisha Wazimbabwe kuhusu michakato ya uchaguzi Picha: Reuters

Wizara ya mambo ya nje ya Zimbabwe ilimwita kaimu balozi wa Marekani Jumanne kwa tuhuma za kuingilia masuala ya ndani kabla ya uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Ubalozi wa Marekani unashutumiwa kwa "kuwafundisha Wazimbabwe kuhusu michakato ya uchaguzi nchini humo", vyombo vya habari vya serikali vinaripoti.

Kampeni ya mitandao ya kijamii inayowahimiza Wazimbabwe kujiandikisha kupiga kura "na kuhakikisha sauti yako inasikika" na "kupiga kura kwa amani" imekuwa ikiendeshwa kwenye kurasa za ubalozi huo.

Kaimu balozi wa Marekani Elaine French alikutana na katibu mkuu wa wizara husika ambapo aliambiwa mwenendo wa ubalozi huo haukubaliki, vyombo vya habari vya serikali vilisema.

Machapisho hayo ya mitandao ya kijamii yalielezwa na wizara hiyo kuwa yanalenga uwanaharakati na kuingilia masuala ya ndani ya Zimbabwe. Iliutaka ubalozi huo "kujizuia kutuma jumbe kama hizo".

Msemaji wa ubalozi huo alisema wanasimama na jumbe zinazotaka amani wakati wa msimu wa uchaguzi.

Rais Emmerson Mnangagwa atawania kuchaguliwa tena kwa mara ya pili katika uchaguzi mkuu ujao ambao tarehe yake haijatangazwa.

Kwa sasa wapiga kura wanakagua daftari la wapiga kura na Chama cha upinzani cha Citizens Coalition for Change (CCC) kimetaka ukaguzi wa daftari hilo ukitaja majina yaliyokosekana.

TRT Afrika