Vita vinapotokea katika maeneo mbali mbali vinaibua mjadala mpana, wa jinsi gani sheria za kimataifa zinatakiwa kulindwa, ambazo ndio msingi mkuu wa kuwalinda wale wasiokuwa na hatia, hasa wanawake, watoto, wazee na kuendelea.
Misingi ya sheria hizi imeanzia mwaka wa 1949 katika mkutano wa kimataifa wa kidiplomasia uliofanya marekebisho katika sheria nyengine za kimataifa za hapo awali. Sheria hizi zilijikita zaidi kuhakikisha usalama wa waathiriwa wa vita .
Mkutano huo ulifanya makongamano manne, ambayo yalipitishwa huko Geneva mnamo Agosti 12, 1949.
Je, sheria hizo za kimataifa za vita ni zipi ?
Kwanza kabisa usalama wa raia wasiokuwa na hatia.
Wakati wowote wa vita, kwa mujibu wa sheria za kimataifa za vita, ni kinyume kushambulia majengo ya kiraia kama makazi, nyumba za ibada, shule na hospitali na miundombinu muhimu kama ikiwemo madaraja, barabara, vyanzo vya umeme na vyanzo vya maji.
Kuua au kumjeruhi mtu ambaye amejisalimisha au hawezi tena kupigana pia ni ukiukaji wa sheria hizo.
Kujali waliojeruhiwa
Waliojeruhiwa na wagonjwa daima wana haki ya kutunzwa na kupata matibabu, bila kujali wapo upande gani wa mgogoro.
Wafanyakazi wa matibabu na misaada ambao wako kazini katika maeneo haya ni sharti kulindwa kwa sababu hawaegemei upande wowote. Waandishi wa habari pia ni katika kundi la watu ambao hawapaswi kushambuliwa.
Uwezo wa watu kuondoka
Pande zote zinazozozana lazima zichukue hatua zote zinazofaa kuhakikisha raia wanaotoka pande zote wanafikiwa na msaada ya kibinaadamu ikiwemo matibabu, chakula, maji au makazi.
Hivyo ni sharti kuwepo kwa makubaliano ya njia salama itakayotumika kwa shughuli hizo.
Pia ni haki ya wananchi kupewa tahadhari ya kuondoka katika maeneo hatari iwapo kuna mpango wa kushambuliwa maeneo hayo. Raia hawapaswi kamwe kuzuiwa kukimbia na kwenda sehemu salama.
Silaha haramu
Kulingana na Mikataba ya Geneva, ni marufuku kwa pande zozote zinazozozana kutumia silaha za maangamizi kama vile mabomu ya nuklia, mabomu ya ardhini, fosforasi nyeupe na kuendelea.
Adhabu ya kukiuka sheria ni nini?
Anayevunja sheria hizi anafaa kushtakiwa katika mahakama ya nchi husika, au Mahakama ya Kimataifa ya Makossa ya Jinai- ICC.
Umoja wa Mataifa unaweza kuunda tume ya kuchunguza tuhuma hizo ili kuchukua hatua stahiki.
Hata hivyo, tafiti zinaonyesha kuwa mara nyingi kumekuwana ukiukwaji wa sheria hizi pindi panapotokea migogoro.