Zanzibar inatafuta wadau na washirika zaidi katika juhudi zake za kuutunza na kuuhifadhi Mji Mkongwe / Picha:TRT AFRIKA

Zanzibar inatafuta wadau na washirika zaidi katika juhudi zake za kuutunza na kuuhifadhi Mji Mkongwe kutokana na umuhimu wake katika kuchangia pato la uchumi wa visiwa hivyo vya marashi ya karafuu.

Wito umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi siku ya Alhamisi 10 Oktoba, alipokutana Ikulu Zanzibar na ujumbe kutoka Taasisi ya “International National Trust Organization” ya Uingereza.

Wajumbe hao walimueleza mafanikio waliyoyapata katika kulifanyia ukarabati jengo la “Custom House” liliopo Forodhani maarufu jengo la Mizingani.

Mji Mkongwe wa Zanzibar ni mfano mzuri wa miji ya Waswahili ya pwani ya Afrika Masharik/ Picha: TRT Afrika

Mkutano huo uliosheheni wataalamu wa masuala ya uhifadhi wa miji ya urithi, ulihudhuriwa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga, pia ulijumuisha taasisi za uhifadhi miji ya urithi kutoka Uingereza, Uganda, Jordan na Misri.

Rais Mwinyi amesema mbali na Mji Mkongwe kuwa katika eneo la Urithi wa dunia, lakini ni muhimu pia katika kukuza kukuza uchumi wa visiwa vya Zanzibar.

Mji Mkongwe wa Zanzibar ni kivutio kikubwa cha utalii/ Picha: TRT Afrika

Kupitia Sekta ya Utalii, fedha nyingi za kigeni zinaingia serikalini kutokana na kuwa eneo linalotembelewa na wageni wengi.

Rais Mwinyi aliweka wazi furaha yake kwa juhudi na hatua zilizochukuliwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe (JUHIMKO) katika kufanya ukarabati mkubwa jengo la Mizingani.

Watu wajitokeze tuulinde Mji Mkongwe

Katika mazungumzo yake Rais Mwinyi, alizitaka taasisi na wadau wengine kujitokeza kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuhifadhi maeneo ya urithi ikiwemo Mji Mkongwe kwani una majengo mengi yanayohitaji ukarabati na kutunzwa kwa fedha na utaalamu.

Naye David Antony Simpson, Meneja Miradi wa Taasisi ya “International National Trust Organization”, akizungumzia changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, amesema kuongezeka kwa kina cha bahari ni miongoni mwa changamoto inayoikabili miji mingi ya urithi duniani iliyoko pembezoni mwa bahari kama ilivyo kwa Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Mji Mkongwe wa Zanzibar ndio kitovu cha kitamaduni cha zamani cha Zanzibar ambayo imekuwezo kwa zaidi ya miaka 200/ Picha: TRT Afrika

Simson, ameahidi kuwa taasisi yake itaendeleza ushirikiano na Zanzibar ili kuhakikisha Mji Mkongwe unabaki kwenye ramani ya dunia.

Taasisi hiyo yenye uzoefu kwa nchi 102 duniani wa kufanya ukarabati wa miji mikongwe, takriban paundi 80,000 ambazo ni zaidi ya Shilingi milioni 280 zilitumika kulifanyia ukarabati jengo la Mizingani chini ya ufadhili wa Mfuko wa Baraza la Urithi la Uingereza

TRT Afrika