Tukio hilo limetokea kisiwani humo, Machi 5, 2024. / Picha: TRT Afrika

Watoto wanane wamepoteza maisha na wengine 78 wamelazwa hospitalini kisiwani Panza, Wilaya ya Kusini, Pemba, Zanzibar, baada ya kula nyama ya Kasa.

Daktari wa eneo hilo, Haji Bakari Haji, amesema Ijumaa kwamba awali, baada ya kufikishwa hospitalini, wagonjwa hao hawakutoa taarifa ya kilichowasibu, hata hivyo baada ya vipimo kuchukuliwa kwa uchunguzi zaidi, ilibainika kuwa walikula nyama ya Samaki aina ya Kasa.

Dk Haji alisema tukio hilo lilitokea Machi 5, 2024, kisiwani.

Jumla ya wagonjwa 86 wamepokelewa hospitalini, na vifo vya watoto wanane vimeripotiwa baada ya wao kula kasa/ picha TRT Afrika

Moja wa waathiriwa, Miza Kombo Bakari aliyepoteza watoto wake katika janga hilo, alikiambia chombo cha habari nchini Tanzania, kuwa aliwakuta watoto wake wakitapika hovyo, na kuamua kuwakimbiza hospitali, kabla hawajafikwa na umauti.

Hii si mara ya kwanza kutokea kwa tukio la kifo linalohusisha vifo vitokanavyo na ulaji wa Samaki huyo.

Mamlaka zimezuia matumizi ya nyama ya Kasa kwa lengo la kuzuia maafa zaidi na kulinda afya ya umma. Picha :  TRT Afrika

Mwaka 2021, watu saba, ikiwa ni pamoja na mtoto wa miaka mitatu, walifariki kisiwani Pemba baada ya kula nyama ya Kasa mwenye sumu.

Licha ya kuwa kitoweo maarufu miongoni mwa wakazi wa visiwa vya Tanzania na maeneo ya pwani, mamlaka zimezuia matumizi ya nyama ya kasa kwa lengo la kuzuia maafa kama haya na kulinda afya ya umma.

TRT Afrika