Huku vita vikiendelea nchini Sudan, kati ya jeshi la Sudan na kikundi cha Rapid Support Forces, watu wanaendelea kuhama makazi yao kwa ajili ya kutafuta usalama.
"Takriban watu milioni 10.7 sasa wamekimbia makazi yao kutokana na migogoro nchini Sudan, huku milioni 9 wakiwa ndani ya nchi hiyo, na kuifanya Sudan kuwa na idadi kubwa zaidi wa wakimbizi wa ndani duniani," Umoja wa Mataifa umesema.
Shirika hilo limesema takriban watu milioni 3.5 wamehama makazi yao katika mji mkuu wa Khartoum peke yake.
Ripoti za Shirika la Chakula Duniani WFP, zinaonyesha kuwa watu milioni 16 nchini Sudan hawana chakula cha kutosha huku eneo la Darfur nchini humo likiwa na changamoto kubwa zaidi.
Changamoto ya magonjwa imeongezeka huku visa vinavyoshukiwa kuwa vya kipindupindu vikiendelea kuongezeka, vikiwemo vifo 292 vilivyohusishwa, na ugonjwa huo viliripotiwa kutoka maeneo 60 ya majimbo 11.
Maafa katika kambi za Darfur
Tathmini ya haraka ya lishe na vifo iliyofanywa na Shirika la Misaada ya Kibinadamu la Médecins Sans Frontières (MSF) inaonyesha kuwa hali ya janga imetokea katika kambi ya Zamzam, Darfur Kaskazini, tangu mzozo nchini Sudan uanze Aprili 2023.
"Hatua ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa - ambayo yamedumisha uwepo mdogo tu huko Darfur Kaskazini tangu walipohama mwezi Aprili - ni muhimu kwa kufanikisha hilo," MSF imesema katika taarifa.
"Ugawaji wa chakula na pesa unahitajika haraka. Huduma ya afya na utoaji wa maji na usafi wa mazingira pia ni muhimu. Takriban robo ya watoto waliochunguzwa wakati wa tathmini hiyo wameonekana kuwa na utapiamlo, huku asilimia saba wakiwa na utapiamlo mkali sana," utafiti huo wa MSF umeonyesha.
Hali mbaya ya dharura katika kambi ya Zamzam huko Darfur inaashiriwa na idadi ya vifo katika kambi hiyo kwa siku pia ilisababisha hofu kubwa, na kiwango cha vifo visivyo vya kawaida vya watu 2 kwa kila watu 10,000 kwa siku - zaidi ya mara mbili ya kipimo cha kawaida cha dharura.
Imani ya vita kumalizika imezidi kudidimia, baada ya majenerali wanaozozana kukosa kuafikiana.
Sudan imejiondoa katika Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo, IGAD , muungano wa nchi nane ambao ulikuwa unaongoza jitihada za kuleta maafikiano kati ya jenerali Abdel Fattah al-Burhan kiongozi wa jeshi la Sudan na jenerali Mohamed Hamdan Dagalo anayeongoza kikosi cha Rapid Support Forces.