Sudan cholera

Mgogoro wa kibinadamu kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan pia unazidisha maambukizi ikiwa ni pamoja na kipindupindu, na ugonjwa wa bakteria umeua zaidi ya watu 300 katika eneo hilo, Afisa wa Afya Duniani alisema Ijumaa.

Afisa wa WHO Margaret Harris alisema katika ujumbe kwa vyombo vya habari kuwa visa 11,327 vya kipindupindu na vifo 316 zimeripotiwa na kwamba homa ya dengue na ugonjwa wa meningitis pia inaongezeka.

"Tunatarajia kuwa visa vitaongezeka zaidi ya ilivyoripotiwa," aliongeza.

Japo afisa huyo wa WHO hakubainisha ni maeneo gani hasa yaliyoathirika na maambukizi hayo, Kipindupindu sio kitu kipya kwa nchi hiyo tangu kuzuka kwa mapigano zaidu ya mwaka mmoja uliopita.

Mnamo Februari 2024, Waziri wa Afya wa Sudan Mohammed Ibrahim alisema kesi za kipindupindu zimetambuliwa katika majimbo 12 kati ya 18 ya nchi hiyo, na kuongeza kuwa idadi ya kesi imefikia 10,800.

Uhaba wa chanjo

Ibrahim alisema kampeni ya chanjo dhidi ya kipindupindu ilianzishwa mwezi Novemba na Desemba mwaka jana lakini kutokana na matatizo ya kiusalama nchini humo, mlipuko huo haukuweza kuzuilika.

Hatari ya sasa hata hivyo imezidishwa kutokana na tisho la magonjwa mengine kama homa ya dengue na Menengitis.

Pia, wiki iliyopita kundi la waasi linalodhibiti Milima ya Nuba nchini Sudan na sehemu za jimbo la Blue Nile lilisema kwamba wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na janga la njaa.

Chama cha Sudan People's Liberation Movement-North (SPLM-N) kilisema kuwa 20% ya familia zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, wakati 30% ya watoto wanakabiliwa na utapiamlo.

Toleo la Kiarabu la taarifa hiyo lilielezea hali hiyo kama njaa.

Ilisema pande zinazohusika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan na mavuno duni ndizo zilizosababisha janga hilo.

Wachunguzi wa kimataifa wanasema kuwa zaidi ya watu milioni 6 wanakabiliwa na uhaba wa chakula kote Darfur, ambayo inadhibitiwa zaidi na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), mpinzani wa jeshi katika vita vya miezi 16, na kwamba njaa imeshika kasi katika kambi ya Zamzam Kaskazini mwa Darfur.

Baraza kuu la Sudan lilisema Alhamisi kwamba litaruhusu matumizi ya kivuko cha mpaka cha Adre na Chad kwa miezi mitatu - hatua iliyosubiriwa kwa muda mrefu na mashirika ya misaada yanayotaka kupeleka misaada katika maeneo ya jimbo la Darfur ambayo yanatishiwa na njaa.

Serikali iliyoshikamana na jeshi ilizuia uwasilishaji wa misaada mwezi Februari kupitia njia ya Adre kuvuka hadi katika eneo linalodhibitiwa na RSF, kwa madai kuwa ilikuwa inatumika kwa kusafirisha silaha.

Sudan imekumbwa na vita kati ya jeshi, likiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, mkuu wa Baraza Kuu la Sudan, na Vikosi vya Msaada wa Haraka vya kijeshi, tangu Aprili. Mzozo huo umesababisha vifo vya watu 5,000 na wengine zaidi ya milioni 5.2 kukimbia makazi yao, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.

TRT Afrika na mashirika ya habari