Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) limesitisha kwa muda msaada wa chakula katika baadhi ya maeneo ya jimbo la Gezira nchini Sudan huku mapigano yakitapakaa kusini na mashariki mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum, shirika hilo la msaada limesema katika taarifa yake.
Takriban watu 300,000 wameukimbia mji wa Gezira katika kipindi cha muda mfupi, tangu mapigano kuibuka Ijumaa wiki iliyopita, imesema WFP.
Usalama kwanza
WFP imesitisha usambazaji wa chakula katika baadhi ya maeneo ya Gezira, amesema Eddie Rowe, mwakilishi wa WFP na mkurugenzi nchini Sudan.
“Tumedhamiriwa kuwasaidia watu wa Sudan katika muda wanaohitaji msaada sana, lakini usalama wa wafanyakazi wetu lazima uhakikishwe.
Watu wetu wanafanya kazi saa 24 kutoa msaada wa chakula katika maeneo ambayo bado yapo salama, inawezekana tutarudia mpango wetu wa msaada katika maeneo mengine pindi kutakapokuwa salama kufanya hivyo," ameongeza kusema Rowe.