Abdiqani Mohamoud Ateye waziri wa ulinzi wa  Somalilandamejiuzulu/ Picha kutokaSomalia Live Update

Waziri wa Ulinzi wa Somaliland amejiuzulu kama ishara ya kupinga mkataba mpya kati ya nchi yake na Ethiopia wa tarehe mosi Januari mwaka huu,

Hii ni kulingana na ripoti kutoka Shirika la Habari la AFP.

Katika mkataba huo, Somaliland imekubali kukodisha kilomita 20 za ukanda wa pwani ya Bahari Nyekundu kwa miaka 50 kwa Ethiopia.

Inaripotiwa Abdiqani Mohamoud Ateye alijiuzulu akisema kuwa mawaziri walipaswa kushauriwa kuhusu mpango huo ambao Somaliland ilifikia na Ethiopia.

Somalia imekataa makubaliano ya bandari ya Ethiopia ya Bahari Nyekundu na Somaliland, na kuyaita "haramu," tishio kwa ujirani mwema na ukiukaji wa uhuru wake. Pia ilimwita balozi wake nchini Ethiopia baada ya mpango huo kutangazwa.

Makamanda wa kijeshi wa Ethiopia na eneo lililojitenga la Somalia la Somaliland walikutana Jumatatu katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa.

Viongozi hao walijadili ushirikiano wa kijeshi huku kukiwa na kuongezeka kwa mvutano kati ya Mogadishu na Addis Ababa baada ya Ethiopia isiyo na bandari kutia saini makubaliano ya awali na Somaliland mapema mwezi huu ambayo yataiwezesha kuingia baharini kupitia bandari ya Bahari Nyekundu ya Berbera.

TRT Afrika