Ramadhan Kibuga
TRT Afrika, Gitega, Burundi
Aliyekuwa waziri mkuu nchini Burundi Alain Guillaume Bunyoni ameiomba mahakama ya nchi hiyo kumuacha huru kwa dhamana kutokana na hali yake ya afya kuzidi kuwa mbaya.
Bunyoni amesema yuko tayari kulipa kiasi cha dola laki moja kama dhamana ili atoke gerezani. Bunyoni anatuhumiwa kwa uhaini na kuhatarisha usalama wa nchi pamoja na kufuja mali ya umma.
Bunyoni amesema anasumbuliwa na maradhi ya kisukari huku akitaja mazingira ya gerezani kuwa sio rafiki.
Kesi ya Bunyoni imesikilizwa katika mahakama kuu katika gereza kuu la Gitega lililopo makao makuu ya kisiasa katikati mwa Burundi.
Hii sio mara ya kwanza kwa Alain Guillaume Bunyoni pamoja na wakili wake kulalamikia mazingira mabovu ya gerezani.
“Ninazuiliwa katika chumbo kidogo chenye milango mitatu iliofungwa kwa kufuli. Kuna polisi wawili wanafuatilia nisisogelewe mtu yeyote yule. Ikiwa litatokea tatizo nikazidiwa, itakuwa vigumu huduma za dharura kunifikia au kuniwahisha hospitalini,'' aliiambia mahakama huku akiiomba kumwachia kwa dhamana kutokana na hali yake ya afya.
''Nasumbuliwa vikali na maradhi ya kisukari. Licha ya kwamba ninatumia dawa lakini hali yangu ya afya inazidi kudorora. Niko tayari kutoa dhamana. Koti tayari imehodhi mali zangu zote. Lakini niko tayari tena kutoa pia franka millioni 300 kama dhamana ilimradi niachiwe huru.''
Kwa upande wake mwendesha mashtaka ameiomba mahakama kutotilia maanani madai na maombi ya mtuhumiwa huyo
Majaji wa mahakama kuu sasa wana saa 48 kukubali au kukataa maombi hayo ya Alain Guillaume ya kutaka kuachiliwa huru kwa dhamana.
Kesi hiyo imesikilizwa chini ya ulinzi mkali ndani na nje ya gereza kuu ya Gitega. Raia waliruhusiwa kuingia kusikiza kesi hiyo lakini baada ya kukaguliwa na kunyang'anywa simu za mikononi.
Alain Guillaume Bunyoni anatuhumiwa kwa makosa ya uhaini, kuhatarisha usalama, kufuja mali ya umma na kutoa matusi dhidi ya rais wa nchi hiyo.
Bunyoni aliwekwa kizuizini tangu mwezi Aprili mwaka huu ikiwa ni miezi sita baada ya kuondolewa kwenye wadhifa wake wa uwaziri mkuu.
Tangu Chama cha CNDD/FDD kufikia madarakani mwaka wa 2005, Alain Guillaume Bunyoni mwenye cheo cha generali wa polisi alishikilia nyashifa muhimu serikalini na alikuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa kiasi cha kuonekana kama kiongozi wa pili muhimu ndani ya utawala wa CNDD/FDD.