Wafanyabiashara wa ngozi nchini Rwanda wanatafuta usaidizi wa kuweza kufanya biashara katika Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) ikizingatiwa kuwa kuna soko ndogo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Sekta hiyo inawekeza kwenye ngozi za wanyama wakubwa kama vile ng'ombe na za wanyama wadogo kama vile mbuzi, kondoo, kulungu, nguruwe, miongoni mwa wengine.
AfCFTA inalenga kuunda soko jumuishi la biashara ya bidhaa na huduma, pamoja na usafiri huru wa watu na biashara.
“Kuna kanuni inasema tusifanye biashara ya ngozi nje ya soko la Afrika Mashariki , EAC, na nchi hizi bado haziwezi kununua ngozi zote tulizonazo kwa sababu soko ni ndogo sana," Jean D'Amour Kamayirese, mwakilishi wa wafanyabiashara zaidi ya 3,000 wa ngozi nchini Rwanda anasema.
" Bado tuna wanunuzi kutoka nchi nyingine za Afrika, Italia na nyinginezo, wanavutiwa na ngozi zetu kwa sababu ya ubora wake. Tunapojaribu kufanya biashara nje ya soko la EAC, tunatozwa ushuru wa asilimia 80," Kamayirese ameongezea.
Anasema wawekezaji wanataka soko zaidi chini ya Eneo Huru la Biashara la Afrika na maeneo mengine ya dunia.
"Kwa sasa kuna zaidi ya tani100 za ngozi katika maduka, ambazo zinaoza kutokana na ukosefu wa soko katika eneo la EAC," amesema.
Mnamo Oktoba 2022, Mpango wa Biashara wa Kuongozwa na AfCFTA ulizinduliwa ambao unafanya majaribio ya biashara ya chini ya mfumo wa AfCFTA kati ya nchi nane ambao ni wanachama.
Hizi ni pamoja na Cameroon, Misri, Ghana, Kenya, Mauritius, Rwanda, Tanzania na Tunisia huku kukiwa na bidhaa 96 zilizotambuliwa.
Bidhaa hizi ni pamoja na chai, kahawa, bidhaa za nyama zilizosindikwa, unga wa mahindi, sukari, pasta, sharubati ya glukosi,na matunda yaliyokaushwa, miongoni mwa bidhaa zingine.