Serikali ya Rwanda inasema inataka kuwasaidia wafugaji kuepukana na hasara inayoweza kutokea siku za usoni. / Picha: Reuters

Kufuatia mfululizo wa matukio ambapo maelfu ya samaki walikosa hewa ya oksijeni na hivyo kusababisha wafugaji kupata hasara mara kwa mara serikali ya Rwanda imeamua kuwaingiza wafugaji wa samaki katika mpango wa bima ya kilimo.

Serikali inasema inataka kuwasaidia wafugaji hao kuepukana na hasara hiyo siku za usoni.

Bima hii itawafaidi wale wanaofanya ukulima wa samaki katika vizimba vilivyopo katika maeneo ya maziwa tofauti.

Tukio la hivi punde zaidi lilitokea Ijumaa, Julai 1, katika Mkoa wa Mashariki ambapo maelfu ya samaki walikufa kwenye Ziwa Muhazi kufuatia kupungua kwa hewa ya oksijeni kutokana na kugeuka kwa maji na kusababisha vifo vya samaki waliokomaa.

Wizara ya Kilimo na Rasilimali za Wanyama imesema kuwa itajumuisha ufugaji wa samaki katika bima ya ruzuku inayoitwa ‘Tekana’ ambayo kwa kawaida inahudumia ng’ombe wa maziwa, nguruwe, kuku na mazao yanayopewa jina la ‘Tekana’.

Maziwa hayo ni Kivu katika Wilaya ya Rubavu, Mkoa wa Magharibi ambako una vizimba 110 na Ziwa Muhazi katika Wilaya ya Rwamagana, Mkoa wa Mashariki, ambapo una vizimba 95.

Wizara ya Kilimo inasema imeanzisha mafunzo kwa wataalamu katika tasnia ya bima, na maafisa wa kitaalamu wa ufugaji wa samaki ambao watafanya tathmini ya hasara endapo uharibifu utatokea.

Huu utakuwa msingi wa kudai malipo, na kuongeza kuwa juhudi za kuhamasisha wafugaji wa samaki zinaendelea kwa sasa.

Wafugaji wa samaki wanashauriwa kuweka vizimba kwenye kina cha zaidi ya mita nane kutoka ufukweni, ili kutoa nafasi ya kutosha kati ya vizimba na kuvisafisha mara kwa mara ili kuruhusu upatikanaji wa oksijeni ya kutosha.

Wizara inasema kuingizwa kwa samaki katika orodha ya bidhaa zinazolipwa na bima hiyo, kumechangiwa zaidi na ombi la wafugaji wanaokabiliwa na hasara kubwa. mabadiliko ya hali ya hewa.

TRT Afrika