Afrika Kusini imeshuhudia dhoruba zikiangusha miundo dhaifu katika vitongoji kando ya kingo za mito. / Picha: AP

Watu wasiopungua saba wamefariki baada ya dhoruba kukumba mkoa wa KwaZulu-Natal ulioko kusini-mashariki mwa Afrika Kusini wiki hii.

Idara ya mkoa ilisema idadi ya vifo kutokana na mafuriko ya ghafla imeongezeka kutoka watu wanne Alhamisi hadi saba baada ya miili mitatu kupatikana karibu na Mto Umbilo katika manispaa ya eThwekwini siku ya Ijumaa.

"Nyumba katika eneo la eThekwini zilipata uharibifu mkubwa, huku nyumba takriban 70 zikiharibiwa kabisa na nyumba nyingine 110 zikipata uharibifu sehemu," idara hiyo ilisema katika taarifa.

"Hii imeathiri jumla ya watu 552, na kuacha watu 151 bila makazi," idara hiyo iliongeza.

Mabadiliko ya hali ya hewa

Kulingana na tathmini za awali, uharibifu mkubwa umeripotiwa kwenye miundombinu ya barabara, umeme, mfumo wa maji taka, na makazi.

"Kama mkoa wa KwaZulu-Natal, tunakabiliwa moja kwa moja na athari halisi za mabadiliko ya hali ya hewa wakati wa msimu wa baridi," idara ya usimamizi wa maafa ya mkoa ilisema.

Msimu wa mvua katika mkoa wa pwani kawaida huanza mwezi Novemba hadi Machi.

Serikali inasema zaidi ya watu 600 wamekufa kutokana na mafuriko mabaya ambayo yamesababisha nyumba na barabara kusombwa mwaka huu.

AA