Takriban watu 64 walihofiwa kufa kufuatia ajali ya boti kwenye mto katika Jimbo la Zamfara kaskazini magharibi mwa Nigeria, maafisa wa eneo hilo walisema Jumamosi.
Mashua ndogo ya mbao iliyokuwa na wakulima 70 ilipinduka ilipokuwa ikiwasafirisha kuvuka mto hadi kufikia mashamba yao karibu na mji wa Gummi Jumamosi asubuhi. Mamlaka za eneo hilo zilihamasisha wakazi haraka kwa ajili ya shughuli ya uokoaji, na baada ya saa tatu, manusura sita walitolewa majini.
"Hii ni mara ya pili kwa tukio kama hilo kutokea katika eneo la Serikali ya Mtaa wa Gummi," alisema Aminu Nuhu Falale, msimamizi wa eneo hilo ambaye aliongoza juhudi za uokoaji.
Aliongeza kuwa timu za dharura zinazidisha msako wao kwa matumaini ya kupata manusura zaidi.
Zaidi ya wakulima 900 wanategemea kuvuka mto kila siku ili kupata mashamba yao, lakini ni boti mbili tu zinazopatikana, mara nyingi husababisha msongamano, alisema mtawala wa jadi wa eneo hilo.
Jimbo la Zamfara ambalo tayari limekumbwa na magenge ya wahalifu wanaotaka udhibiti wa rasilimali za madini, nalo limeathiriwa pakubwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa.
Wiki mbili zilizopita, mafuriko yaliwahamisha zaidi ya wakazi 10,000, maafisa wa eneo hilo walisema.