Badala ya mazingira ya kawaida ya sherehe na taa za Ramadhan, Wapalestina huko Gaza wameswali sala yao ya kwanza ya tarawehe katika misikiti iliyoharibiwa, mahema ya muda na kambi.
Wakiwa wamesimama kwenye safu nyuma ya imamu huku wamekunja mikono yao, wanaume wa Kipalestina wameingiliwa na mwezi wa kufunga tofauti na vile wamezoea hapo awali.
Na wengine wengi waliokuwa hawakwenda kuswali, walikuwa mitaani wakitafuta chakula chochote wangepata kwa ajli ya kulisha familia zao wanaoishi katika mahema ya muda katika eneo liloharibiwa na vita.
“Natamani ndege zitushambulie kwa bomu na nife," amesema Zaki Hussein Abu Mansur, aliemiliki nyumba alioijenga mwenyewe kwa ajili ya familia yake katika eneo la Khan Yunis – walipokuwa jeshi la Israeli wakifanya oparesheni ya ardhini dhidi ya kundi la wapiganaji wa Hamas.
“Ni bora kufa kuliko kuishi maisha haya,” alisema mzee huyo mwenye miaka 63 kwa AFP, "Mara nyingine tunakuta vitu tunavyohitaji sokoni lakini hatuwezi kuvinunua."
Ukosefu wa vitu ni wa kawaida huko Gaza mwaka huu wa Ramadhani. Masoko huko Rafah yanakosa bidhaa za chakula na maduka machache yana “qatayef”, kitafunio kinachouzwa kawaida wakati wa Ramadhani.
Taa za kungara na mapambo ambayo kawaida hupamba mitaa wakati wa mwezi wa kufunga yamekosekana, ingawa baadhi ya vibanda wanawasha taa za Ramadhan.
"Hatuna uwezo wa kununua hata mboga, wachana na hata matunda," alisema Maisa al-Balbissi, mwenye umri wa miaka 39 aliyeohamishwa kaskazini mwa Gaza na sasa akiwa huko Rafah.
"Kila kitu ni ghali sana. Watoto wangu na mimi hatuwezi kununua chochote. Bei za vitu hata vya kawaida zimepanda kwa kasi," mama wa watoto wawili alisema kwa mahojiano na AFP akiwa karibu na hema lake.
'Hatuhisi furaha'
Wapalestina wanasherehekea Ramadhan mwaka huu katikati ya mashambulizi makali na uvamizi ulioanzishwa na Israeli.
Kwa wale wanaolazimika kubaki katika kambi zilizojaa watu waliokimbia, ukweli wa wazi wa kukosekana kwa chakula na mazingira machafu ya kuishi kumepunguza furaha ya sherehe ya mwezi mtakatifu.
Takriban watu milioni 1.5 wamekimbilia Rafah, kulingana na Umoja wa Mataifa, huku wengi wakiwa bila chakula, maji, na dawa.
"Ninasumbuliwa na kisukari, shinikizo la damu, na matatizo ya moyo," alisema Abu Mansur, akielezea mapambano yake ya kila siku ya kupata dawa."Siwezi kula vyakula vya makopo."
Licha ya Israel na Misri kuifungia Gaza kwa muda mrefu, katika miaka iliyopita bidhaa zinazohitajika kwa Ramadhani zilikuwa bado zinapatikana.
"Ramadhani hii ni tofauti na mwaka jana ambapo kila kitu kinachohusiana na Ramadhan kilikuwa kinapatikana — iwe ni umeme, chakula, maji," aliiambia Abdelrahman Ashur, mwenye umri wa miaka 19."
"Hakuna kitu kinachopatikana tena. Hatuhisi furaha. Kila Ramadhani tulikuwa nyumbani na sasa tunaketi katika mahema tuliyoyajenga kwa mikono yetu wenyewe,"
'Mtihani wa kweli' unakuja
Jua lilipochomoza siku ya kwanza ya Ramadhani, moshi wa mashambulizi ya anga ulikuwa wazi juu ya Rafah.Awni Al Kayyal, mwenye umri wa miaka 50, alisema aliona magari ya ambulensi yakibeba miili iliyokufa mara tu alipoamka.
"Kuanza kwa Ramadhan kumekuwa na huzuni na uliofinikwa na giza, na harufu ya damu na na uvundo kila mahali... Nilipoamka katika hema langu, nilianza kulia kwa hali yetu," aliiambia AFP.
Jumapili jioni, waumini walifanya sala ya jioni katika msikiti wa Al Hadi, ulioharibiwa katika shambulio la Israeli.
Matao yake ya Kiislamu sasa yamepasuka na kuwa na nyufa, huku nguzo za zege zinazosaidia dari ndani zikiwa zimejipinda kwa njia ya hatari.
Kulingana na ofisi ya vyombo vya habari ya serikali ya Gaza, vikosi vya Israeli vimelenga zaidi ya misikiti 500 tangu mwanzo wa vita, na 220 kati yao yameharibiwa.Wakati huo huo, huko Jerusalem Mashariki iliyokaliwa kwa mabavu, hofu ya mapigano wakati wa Ramadhan inaendelea kati ya Wapalestina.
Kila mwaka, makumi ya maelfu ya Waislamu hufanya sala ya Ramadhani kwenye msikiti wa Al Aqsa, eneo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu.
Mwaka huu Hamas imetoa wito kwa "watu wetu" kuhamasishwa na kuandamana kuelekea Al Aqsa kuanzia mwanzo wa Ramadhani."Kwa sasa kuna utulivu.
Tutaona siku ya Ijumaa," Ali, mkazi wa Jiji la Kale, akirejelea swala ya Ijumaa, wakati mikusanyiko mikubwa inapokusanyika msikitini. "Huo utakuwa (mtihani) halisi," alisema.