Mwaka mpya umeanza vyema kwa wapagazi juu ya Mlima mrefu kuliko yote Afrika kufuatia la nyongeza ya mishahara yao.
Kwa mujibu wa kiongozi wa Chama cha Wapagazi Tanzania (TPO) Loishiye Mollel, malipo yao yamepanda kutoka fedha za Kitanzania 2,000 had 25, 000.
Mabadiliko hayo yanafuatia harakati za muda mrefu zilizowashirikisha TPO na Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), idara ya kazi pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
"Hii ni habari njema kwetu, hasa ukizingatia mahali tulipotoka," anatabanaisha Mollel, katika mahojiano maalumu na TRT Afrika.
Kiongozi huyo wa wapagazi wanaofanya kazi ya kubeba mizigo ya watalii pindi wanapopanda mlimani, anakiri kwamba kiwango cha awali kilikuwa ni cha chini mno kwa mtu kuweza kujikimu kimaisha.
Hata hivyo, mabadiliko haya mapya yanatarajiwa kufikia kikomo mwisho wa mwaka huu, wakati ambapo wapagazi hao wanatarajia kukaa mezani na makampuni ya waongoza utalii kupitisha mapendekezo ya malipo mapya ya 30,000.
Kulingana na Mollel, mpagazi juu ya mlima huo atakuwa amejihakikishia kiasi cha shilingi 250,000 kwa safari moja ambayo inachukua takibani siku kumi, kwa malipo ya shilingi 25,000 kwa siku.
“Namna hii tutaweza hata kuomba kuanganishwa kwenye bima ya afya kwa kiwango cha chini kabisa cha laki moja,” anaongeza.
Mwaka 2008, serikali ya Tanzania, kupitia tangazo lake number 22, iliongeza mishahara ya wagumu na kufikia dola 20,000 kwa siku, japo bado kulikuwa na baadhi ya kampuni za mawakala wa utalii waliokuwa wanalipa chini ya kiwango hicho kilichopitishwa na watunga sheria.
Kuelekea mlimani, wapagazi hubeba mzigo yenye uzito wa kuanzia kilo 20, kwa nyakati za masika hata kiangazi.