Idadi ya watu nchini Afrika Kusini iliongezeka hadi watu milioni 62 mwaka jana kutoka milioni 51.8 mwaka 2011, kulingana na takwimu za sensa kutoka kwa wakala wa takwimu.
Takwimu zilionyesha wanawake wengi walipata sifa ya elimu ya juu kuliko wanaume nchini Afrika Kusini katika kipindi hicho, licha ya takwimu za hivi karibuni kuonyesha kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira kwa wanawake kuliko wanaume.
Sensa hiyo ilipata takriban watu wanane kati ya 10 walikuwa waafrika mnamo 2022, wakati chini ya mtu mmoja kati ya 10 walikuwa wazungu.
Takwimu za Afrika Kusini zilisema kulikuwa na zaidi ya wahamiaji milioni 2.4 nchini Afrika Kusini mwaka jana, huku asilimia kubwa zaidi wakitoka nchi jirani ya Zimbabwe wakiwa 45.5%, ikifuatiwa na Msumbiji na Lesotho.
Sensa ya nne
"Uhamiaji kati ya nchi unasukumwa kwa kiasi kikubwa na utafutaji wa fursa za kiuchumi, kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na kuongezeka kwa hatari za kimazingira," ilisema ripoti ya shirika la Stats SA.
Hii ilikuwa sensa ya nne tu tangu uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia baada ya kumalizika kwa ubaguzi wa rangi mwaka 1994, na ya kwanza katika kipindi cha muongo mmoja kutokana na kukatika kwa ukusanyaji wa data kulikosababishwa na janga la COVID-19.
Kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini, sensa ilifanyika mtandaoni kabisa.
Rais Cyril Ramaphosa alipongeza wakala wa takwimu kwa hili, akiongeza kuwa taarifa hizo ni muhimu kwa mipango ya serikali.
"Itatusaidia kufahamisha jinsi bajeti inapaswa kupangwa," alisema Ramaphosa katika mkutano na wanahabari kufuatia kutolewa kwa sensa hiyo, akiongeza kuwa data hizo pia zitafahamisha jinsi rasilimali za nchi zitakavyotumika na kusambazwa.
Upatikanaji wa makazi
Kulikuwa na uboreshaji wa upatikanaji wa nyumba bora kwani takwimu zilionyesha ni asilimia 8.1 tu ya familia zilizoripotiwa kuishi katika makazi yasiyo rasmi mwaka 2022 ikilinganishwa na 13.6% mwaka 2011.
Hata hivyo, taarifa zinazohusiana na mali za familia - kipimo cha hali ya maisha nchini - zilirudishwa nyuma katika sensa hii kutokana na ukosefu wa takwimu za kutosha.
Data nyingine ambazo bado hazijakamilika ambazo kwa kawaida ni sehemu ya sensa hiyo ni pamoja na mgawanyo wa mapato na utajiri, vifo na ukosefu wa ajira, vipimo vyote muhimu vinavyoonyesha kama nchi imepunguza umaskini na ukosefu wa usawa.
Afrika Kusini itafanya uchaguzi wake wa kitaifa mwaka ujao na takwimu za hivi punde za sensa zitakuwa fundisho kwa mashirika yote ya kisiasa na serikali yanayotaka kutatua changamoto zinazoikumba nchi hiyo.