Muhammadu Buari alishika hatamu ya Urais wa Nigeria mwaka 2015; Picha AFP

Rais anayeondoka wa Nigeria Muhammadu Buhari alichaguliwa 2015 katika uchaguzi wa kipekee, alipopata umaarufu mkubwa na kuungwa mkono kwa kiwango cha juu na kumpiku mpinzani wake ambaye alikuwa rais wakati huo Goodluck Jonathan wa chama Peoples’ Democratic Party.

Kama kiongozi wa chama cha maendeleo ya watu APC, Buhari alikuwa rais wa kwanza kuwahi kumshinda rais aliye madarakani katika uchaguzi nchini Nigeria. Aliahidi kukabiliana na ukosefu wa usalama, kupiga vita ufisadi na kuimarisha uchumi.

Wakati huo, wasi wasi mkubwa mionmgoni mwa wananchi wa Nigeria na jamii ya kimataifa ulikuwa vurugu za Boko Haram zilizokithiri, huku kundi hilo la wapiganaji likiendelea kuteka maeneo ya mengi nchini Nigeria, mashambulio ya mabomu na utekaji nyara wa watu kila uchao.

Uimarishwaji wa jeshi

Huku rais Buhari akiondoka baada ya miaka minane uongozini, serikali yake inajivunia mafanikio katika kukomboa maeneo yaliyokuwa chini ya Boko Haram na kuwa ‘imevunja nguvu’ kundi hilo pamoja na washirika wake ISWAP.

Mzozo huo ulioanza 2009 umesababisha vifo vya watu 350,000 , kwa muijbu wa shirika la Umoja wa Mataifa.

Akihutubia kongamano la kukabiliana na ugaidi mwezi Machi, Rais Buhari alisema kuwa ufanisi dhidi ya Boko Haram na makundi mengine yaliyojihami ulifikiwa hasa kutokana na juhudi za vikosi vya uslama vya Nigeria kwa ushirikiano na washirika wake katika eneo hilo pamoja na raia wa Nigeria.

Vikozi vya Nigeria vimekuwa vikipigana na Boko Haram kwa miaka mingi Picha AFP

Ukosefu wa vifaa muafaka vya kijeshi umekuwa mojawapo ya changamoto kubwa katika vita dhidi ya Boko Haram. Lakini serikali ya Buhari iliweza kununua silaha zaidi zikiwemo ndege za kivita 38 za kikosi cha wanahewa cha Nigeria.

‘’Ufanisi wa Nigeria katika kununua silaha umesaidia sana kupigana na ugaidi,’’wakili wa Nigeria, Idris Bawa ameambia TRT Afrika.

Japo Boko Haram imekatwa makali yake, makundi yaliyojihami yameendelea kupata nguvu na kuwateka watu nyara kwa ajili ya kudai vikombozi hasa katika maeneo ya kaskazini mwa nchi, huku yakilenga wasafiri, watoto wa shule na wakaazi wa vijijini na kuwaathiri maelfu ya watu katika miaka mitatu iliyopita.

Lakini rais anayeondoka Muhammadu Buhari ambaye aliwahi kuwa mkuu wa jeshi, amesema kuwa juhudi zinafanyika kukabiliana na makundi ya utekaji nyara ambao wamekuwa wakiitwa mitaani kama ‘majangili.’

Japo uchumi wa Nigeria unaotegemea pakubwa uzalishaji wa mafuta umekabiliwa na wakati mgumu huku thamani ya sarafu yake ikiyumba na kusababisha mfumko wa bei, uongozi wa Buhari umefanikisha juhudi nyingi za kupunguza umaskini, kuimarisha kilimo na usambazaji wa umeme.

Mageuzi ya sekta ya mafuta

Serikali imelaumu baadhi ya changamoto hizi kwa kushuka kwa bei za mafuta kimataifa na athari kubwa ilityotokana na janga la Covid 19. Alisema kuwa uchumi sasa unaelekea kuimarika licha ya ukuaji wa polepole wa pato la taifa.

Chini ya uongozi wa Buhari, Nigeria imepata hali ya utulivu katika eneo linalozalisha mafuta la Niger Delta ambako makundi ya wapiganaji yanayotafuta mgao kutoka kwa mafuta hayo yamekuwa yakishambulia vituo vya mafuta, kuiba mafuta na kuwateka nyara wafanya kazi.

Miradi ya kuchimba mafuta pia ilianzishwa kaskazini mwa nchi kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi.

Serikali ya Buhari pia imeleta sheria mpya iliyofanyia mabadiliko makubwa sekta ya mafuta 2021.

Sheria hiyo ya kusimamia viwanda vinavyozalisha mafuta, inashinikiza uwepo wa uwekezaji zaidi wa kibinafsi katika sekta ya mafuta na kutoa hisa zaidi kwa jamii zilizo maeneo ya kuzalisha mafuta .

Bwana Buhari amesema kuwa taifa limepoteza zaidi ya dola bilioni 50 katika uwekezaji katika miaka kumi iliyopita kutokanana kucheleweshwa kupitishwa sheria hiyo na serikali zilizotangulia.

Nigeria imeongeza uwekezaji katika sekta ya mafuta kwa miaka mingi. Picha UGC        

Kutokana na sheria hiyo, kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali, Nigerian National Petroleum Corporation, imegeuzwa sasa kuwa kampuni ya Limited Liability, kumaanisha kuwa, wamiliki wa hisa sasa hawatabeba mzigo wa hasara zinazotokana na kampuni. Hii inanuiwa kuwavutia waekezaji zaidi wa kibinafsi.

Hatua hiyo imepongezwa na wengi akiwemo Babatunde Azeez, meneja wa kituo cha mafuta mjini Lagos.

Hata hivyo bwana Azeez anasema kuwa hakuridhishwa na baadhi ya sera za kiuchumi ikiwemo kufungwa kwa mipaka ya nchi kwa miezi kadhaa, 2019 na 2020, hatua ambayo anasema iliathiri biashara nyingi sana, hasa wale wanaouza kwa kuvuka mipaka.

“Tunaweza kuona sababau za serikali kuchukua hatua hizo, mfano wakati wa janga la Covid-19, kuporomoka kwa uchumi au athari za vita vya Urusi na Ukrain. Lakini kuna mambo ambayo hayawezi kubalika kama kufungwa kwa mipaka.’’ Aliambia TRT Afrika.

Hata hivyo serikali inasema kuwa kufungwa kwa mipaka kulisaidia kudhibiti hali ya usalama na mauzo ya bidhaa bandia na silaha.

Serikali pia imesema hatua hiyo ilisaidia kuzalisha chakula cha ndani kwani kulipunguza kuingizwa bidhaa za nje na kuliimarisha kilimo cha ndani.

Sifa nyingine ya Rais Buhari ni kufufuliwa kwa mfumo wa usafiri wa reli nchini ikiwemo safari kutoka mji mkuu Abuja hadi mji wa kaskazini wa Kaduna, na nyingine kutoka mji wa Lagos hadi Ibadan, Kaskazini Magharibi na kutoka Itakpe, hadi Warri, katika eneo linalozalisha mafuta la Delta.

Usafiri wa treni kutoka Abuja kwenda Kaduna ulisimamishwa kutokana na shambulio la watu wlaiojihami Picha AFP

“Ufufuaji wa usafiri wa reli wa Buhari, umerahisisha maisha kwa wasafiri wengi,’’ amesema Ibrahim Halilu Abubakar, anayesafiri mara kwa mara kwa treni kati ya Kaduna na Abuja tangu 2016.

Abubakar ameambia TRT Afrika kuwa, japo watu waliokuwa na silaha walishambulia treni ya abiria na kuwateka nyara watu kadhaa mwaka jana, kwa kiasi kikubwa, ‘ usafiri wa treni ulitupatia afueni wakati barabara zilikuwa hatari’’ kutokana na utekaji nyara.

Kuondolewa hatari ya ufisadi

Serikali pia imejisifia utengenezaji wa barabara, daraja na kuimarishwa bandari zake, viwanja vya ndege pamoja na sekta ya afya.

Katika sekta ya elimu, iliongeza idadi ya vyuo nchini kutoka 122 hadi 228 – ikiwa idadi kubwa zaidi kuwahi kuwa nayo.

Serikali pia imesema kuwa imeweza kuimarisha usajili wa watoto shuleni.

Lakini serikali pia imekumbwa na migomo mirefu zaidi ya wahadhiri wa vyuo vikuu katika historia ya nchi, iliyowaacha zaidi ya wanafunzi milioni mbili wakihangaika bila masomo kwa miezi minane, 2022.

Wanachama wa muungano wa wafanyakazi wa vyuo, walianzisha mgomo huo wakidai mazingira bora ya kazi na kuongezwa ufadhili kwa vyuo.

Rais Buhari alipoteuliwa, kauli mbiu yake ilikuwa, ‘Tusipoangamiza ufisai, ufisadi utaiangamiza Nigeria.’’

Hii ilikuwa kati ya ahadi zake kupiga vita balaa la ufisadi ambalo alisema kuwa ni tisho la wazi kwa Nigeria.

Waziri wa haki Abubakar Malami alinukuliwa na vyombo vya habari vya ndani mwezi Novemba akisema kuwa tangu 2015, serikali imefanikiwa kurudushia zaidi ya dola bilioni moja zilizoibwa, katika juhudi zake kudhibiti ufisadi.

Wanasiasa wakuu wakiwemo maseneta na baadhi ya magavana wa zamani walikamatwa na kufungwa jela kuhusiana na visa vya ufisadi, katika hatua iliyoonekana kuwa ya kipekee.

Lakini kuachiliwa kwa magavana wawili wa zamani waliokuwa wamekamatwa, Joshua Dariye wa jimbo la Plateau na Jolly Nyame wa Taraba, kumeshutumiwa sana na wanaharakati wa kupiga vita ufisadi waliodai kuwa hatua hiyo imevuruga shguhuli ya kukabiliana na ufisadi.

Serikali ilitetea uamuzi wake na kusema kuwa wanasiasa hao waliachiliwa kutokana na kuzorota kwa afya zao.

‘‘Hatua hiyo ilikuwa hatima ya shughuli ndefu iliyofanywa kwa kuzingatia sheria na wala haikulenga kupata manufaa yoyote kisiasa.’’ Garba Shehu alieleza katika taarifa baada ya kupokea tuhuma kutoka kwa wananchi.

Serikali ya Buhari imeimarisha na kufanyia mabadiliko sheria za kudhibiti ufisadi ili kuwezesha kutaifisha mali za watuhumiwa wa ufisadi zilizoko ndani na nje ya nchi.

Benki kuu ya Nigeria ilianzisha mwezi Februari utekelezaji wa sera za kuzindua sarafu mpya na kuondoa zile za zamani katika hatua inayonuiwa kupunguza ufisadi na kukabiliana na mfumko wa bei na usalama.

Lakini wananchi wengi wa Nigeria akiwemo meneja wa kituo cha mafuta Babatunde Azeez walishutumu sana hatua hiyo wakisema kuwa imesababisha uhaba wa pesa katika masoko jambo lililopekea mahakama kusimamisha shughuli hiyo kwa muda.

Foleni zilionekana katika mabenki ya Nigeria baada ya serikali kutangaza kubadilisha sarafu ya nchi Picha Reuters 

Sheria nyingine muhimu iliyo tiwa saini na rais Buhari ni sheria ya kuzuia ubaguzi wa watu wanao ishi na ulemavu ya 2018, inayowapa watu hao haki zaidi na uhuru wa kuajiriwa popote na kupiga vita unyanyapaa katika ngazi zote kitaifa.

Kujikagua na kuomba msamaha

Wakili wa Nigeria Idris Bawa, amesema kuwa mabadiliko haya ni muhimu kwa taifa kusonga mbele. Pia alitaja madiliko yaliyolenga kuimarisha mfumo wa haki nchini na masuala ya jeshi la polisi kufuatia maandamano ya 2020 dhidi ya ukatili wa polisi yaloyokuja kufahamika zaidi kama maandamano ya EndSARS.

Bawa amesema kuwa serikali ya Buhari ilifanya vyema katika hilo kwani kwa miaka mingi. ‘hatujaona mageuzi kama haya.’

Katika hotuba kwa taifa kabla ya kumalizika muda wake, Rais Buhari aliipatia serikai yake alama za juu katika utenda kazi upande wa kufufua uchumi, kukabiliana na ukosefu wa usalama na kupiga vita ufisadi, kuunganisha wananchi kupitia demokrasia na maendeleo ya miundo mbinu pamoja na kusafisha sura ya Nigeria kwa jamii ya kimataifa.

Licha ya shutuma dhidi ya serikali yake, rais anayeondoka wa Nigeria amesema kuwa: ''nina hakika kuwa naondoka ofisini nikiacha Nigeria bora mwaka 2023 kuliko nilivyoingia 2015.''

Serikali ya Nigeria ilionesha milima ya mchele wake kuonesha kuimarika uchumi na kilimo Picha AFP

Hata hivyo aliwataka radhi wananchi kwa baadhi ya sera za serikali alizosema kuwa ziliwasababishia machungu kwa kuda lakini hayangeweza kuepukika.

Alisema kuwa hatua hizo zilichukuliwa kwa manufaa ya taifa na kuongeza kuwa nyingi ya sera hizo zilifanikiwa kufikia malengo yake.

Buhari alimtakia rais mpya anayeingia Bola Ahmed Tinubu kila la kheri anaposhika usukani wa taifa.

TRT Afrika