Wananchi wa Namibia wanapiga kura siku ya Jumatano kumchagua rais mpya na wabunge katika uchaguzi ambao unaweza kuwa mgumu kwa chama tawala cha SWAPO, ambacho kinataka kurefusha utawala wake wa miaka 34.
SWAPO imetawala taifa hilo la kusini mwa Afrika tangu lilipoongoza kwa uhuru kutoka kwa utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini mwaka 1990. Mgombea wake wa urais, Makamu wa Rais, Netumbo Nandi-Ndaitwah, atakuwa kiongozi wa kwanza mwanamke nchini humo iwapo atashinda.
Wachambuzi wa kisiasa wanasema kuwa ukosefu mkubwa wa ajira, ukosefu wa usawa na madai ya rushwa yamesababisha kutoridhika na chama tawala, hasa miongoni mwa vijana, lakini uaminifu wa muda mrefu kwa SWAPO miongoni mwa wapiga kura wazee na wa vijijini unaweza kukisaidia chama hicho kushinda.
"Ni uchaguzi wenye mvutano zaidi tangu uhuru," alisema Henning Melber, mshiriki katika Taasisi ya Nordic Africa na mwanachama wa muda mrefu wa SWAPO, ambaye alisema kuwa kwa mara ya kwanza, anaona uwezekano wa chama tawala kuweza kushindwa.
Njia ya kushinda
Anayeongoza kundi la wagombea 14 wa upinzani ni daktari wa meno aliyegeuka kuwa mwanasiasa Panduleni Itula, ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita wa 2019.
Namibia kwa sasa inaongozwa na rais wa mpito Nangolo Mbumba, ambaye alichukua madaraka mwezi Februari baada ya rais wa zamani Hage Geingob kufariki. Ijapokua yeye si miongoni mwa wanaokipigania kiti cha urais.
Ili kuchaguliwa kuwa rais, mgombea lazima apate zaidi ya 50% ya kura, vinginevyo kutakuwa na duru ya pili ya upigaji kura.
Wananchi wa Namibia pia wanapigia kura ya kuwachagua wabunge. Takriban watu milioni 1.4 wamejiandikisha kupiga kura katika nchi hiyo yenye wakazi wachache ya karibu milioni 3, kulingana na tume ya uchaguzi.
Matokeo yanatarajiwa ndani ya siku chache.