Umoja wa Mataifa ulisema mnamo Juni 2023 kwamba ujumbe wake wa kulinda amani utaondoka Mali. Picha: AA

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali siku ya Jumapili kilisema kuwa kimeharakisha mpango wa kujiondoa katika mji wa Ber ulioko kaskazini mwa Mali kutokana na kuzorota kwa usalama, huku mapigano katika eneo hilo yakizusha hofu ya kufufuliwa kwa vuguvugu la watu wanaotaka kujitenga.

Katika siku chache zilizopita, muungano wa waasi wa kaskazini unaoongozwa na Tuareg, unaoitwa Coordination of Azawad Movements (CMA), umeshutumu vikosi vya Mali na wanajeshi wa Urusi Wagner kwa kukiuka usitishaji vita kwa kushambulia vikosi vyake vilivyowekwa karibu na Ber.

Jeshi la Mali halijajibu madai hayo, lakini siku ya Jumamosi lilisema wanajeshi wake sita walioko Ber waliuawa wakizuia jaribio la uvamizi lililofanywa na "makundi ya kigaidi yenye silaha."

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaojulikana kwa jina la MINUSMA ulisema katika taarifa yake kuwa "umeharakisha kujiondoa kutoka Ber kutokana na kuzorota kwa usalama."

"Inazitaka pande zote zinazohusika kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kutatiza operesheni," ilisema, bila kutaja waliohusika.

Mashambulio ya waasi

Mapigano hayo yanafuatia madai ya Mali ambayo hayakutarajiwa mwezi Juni kwa MINUSMA kusitisha misheni yake ya muongo mmoja, na hivyo kuzua wasiwasi kwamba kuondoka kwake kunaweza kuleta hitilafu zaidi katika makubaliano ya amani ya mwaka 2015 na waasi wa Tuareg na kudhoofisha juhudi za kukabiliana na uasi wa Kiislamu.

Mapigano kati ya vikosi vya CMA na wanajeshi wa Mali karibu na Ber yalikuwa yakiendelea kuanzia Jumapili asubuhi, msemaji wa CMA Mohamed Elmaouloud Ramadane aliiambia Reuters kwa njia ya simu.

Kuwepo kwa walinda amani wa MINUSMA kumesaidia kuwatuliza waasi wanaoongozwa na Tuareg, ambao walisimamisha uasi wao wa kujitenga na Mkataba wa Algiers wa 2015.

Machafuko katika eneo hilo yalianza nchini Mali mwaka 2012, wakati Waislam walipoteka nyara uasi wa Tuareg. Waasi hao wa Kiislamu tangu wakati huo wameenea katika nchi jirani za Burkina Faso na Niger, na kuua maelfu ya watu na kuwafanya mamilioni ya watu kuyahama makazi yao katika moja ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani.

TRT Afrika