Takriban watu 1,741 kwa siku wanakimbilia Sudan Kusini kutoka Sudan/ Picha: Others 

Mashirika ya kibinadamu yanaripoti ongezeko ya wakimbizi kutoka Sudan kuelekea nchi jirani ya Sudan Kusini.

Vita nchini Sudan ilianza tarehe 15 Aprili mwaka huu baina ya jeshi la taifa la Sudan na kikundi cha Rapid Support Forces.

"Kufikia tarehe 6 Oktoba watu 302,838 wamerekodiwa katika vituo vya kuvuka mpaka, na wengi wao wakifika kupitia maeneo ya Joda/Renk," Ofisi ya Umoja wa Mataifa imesema.

Hii inaashiria takriban watu 1,741 kwa siku wanakimbilia Sudan Kusini, wengi wao wakiwa wananchi wa nchi hiyo waliokimbia vita nchini humo tangu mwaka 2013.

Sudan Kusini yenyewe inaendelea kukabiliwa na migogoro mingi ya kindani.

Ukosefu wa usalama, ghasia za kindani, changamoto za kiuchumi za kikanda na kitaifa zinazochangiwa na kuzorota kwa uchumi wa dunia, athari za mabadiliko ya hali ya hewa na mzozo unaoendelea wa Sudan, vyote vinaathiri vibaya usalama wa chakula kwa watu na haswa familia za watu wa Sudan Kusini.

Shirika la Médecins Sans Frontières (MSF) linatoa wito wa dharura wa kuboreshwa kwa matibabu na misaada ya kibinadamu kwa watu wanaokimbia vita nchini Sudan na kuingia Sudan Kusini kupitia Renk, mji ulioko kaskazini mwa jimbo la Upper Nile.

Hali yazorota

Watu wa Sudan pia wamekabiliwa na mshtuko zaidi katika wiki za hivi karibuni kwani mvua kubwa na mafuriko yameathiri zaidi ya watu 70,000 katika majimbo saba, na kusababisha wasiwasi wa kuongezeka kwa magonjwa yanayosababishwa na maji.

Umoja wa Mataifa unasema mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu umetangazwa katika jimbo la mashariki la Gedaref na wahudumu wa kibinadamu tayari wanachunguza iwapo umeenea hadi Khartoum na Kordofan Kusini.

"Huku mapigano yakiongezeka, inaweza kuwa vigumu kudhibiti maafa mengien yanayojitokeza," amesema Clementine Nkweta-Salami, Mratibu Mkazi wa Misaada ya Kibinadamu nchini Sudan.

Nkweta-Salami ameongezea kuwa nusu ya wakazi wa Sudan, takriban watu milioni 24.7 sasa wanahitaji usaidizi wa kibinadamu na ulinzi, akionya kuwa migogoro, uhamisho na milipuko ya magonjwa sasa "inatishia kuiteketeza nchi nzima".

Ametoa wito kwa pande zinazopigana kujitolea tena kwa ahadi za awali za "kukomesha mapigano, kupunguza madhara ya raia na kujiepusha na mashambulizi yoyote yasiyo na uwiano" .

Pande mbili zinazozozana nchini Sudan bado hazijaonyesha hamu ya kufanya maafikiano yoyote rasmi au kukomesha vita.

TRT Afrika