Ronald Sonyo
TRT Afrika, Katesh, Tanzania
Mji wa katesh bado unapambana kurudisha hali ya mji huo baada ya mafuriko ya siku kadhaa zilizopita kusababisha maafa makubwa na kuua watu zaidi ya 65 na kusambaratisha makazi ya zaidi watu elfu tano.
Janga hilo lilivikumba vitongoji vya karibu vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay na Sebasi, vyote vikiwa katika wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara.
Katesh ni miongoni mwa miji maarufu nchini Tanzania, ambapo wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hufanya biashara hasa za nafaka katika mji huo. Hata hivyo, baada ya janga hilo lililotokea mwishoni mwa juma, taswira imekuwa tofauti kwa wanaoujua mji huo. Hivi sasa kinachoonekana mjini humo, ni huzuni, na sura zilizojawa na huzuni kutokana na vifo vilivyotokea, majeruhi pamoja na hasara ya mali na miundombinu iliyosababishwa na maporomoko hayo.
Huduma muhimu za kijamii, ikiwemo umeme na maji ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika. Wakati serikali serikali ikiendelea kupambana kurudisha huduma hizo, kwa siku kadhaa wengi watasalia bila kupata huduma hizo za msingi.
Mafuriko haya yamebadili kabisa taswira ya mji kutoka tambarare hadi kuonekana kama sehemu iliyomwagikiwa na volcano. Kinachoonekana hivi sasa ni mawe makubwa, magogo ya miti na mabaki ya vyombo vya ndani, kama vitanda, magodoro na meza zilizokatika ambavyo vyote vilikuwa sehemu ya msafara wa matope. Mbali na hayo, pia kuna harufu kali itokanayo na vyakula kama dagaa na samaki, pamoja na nafaka.
Ingawa Serikali ya Tanzani kupitia agizo la rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan imeelekeza nguvu nyingi katika mji huo ikiwa ni pamoja na kutuma kikosi cha kupambana na maafa kilichopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuokoa watu na kurekebisha miundombinu iliotahirika, lakini baadhi ya wakazi wa eneo hiyo wanasema huenda ikachukua muda kwa hali kurudi kama ilivyokuwa.
Simon Sule akiwa amekaa juu ya mbao zilizokatika huku akikumbuka jinsi mafuriko hayo yalivyoua ndugu na jamaa zake. “Nilipomaliza kujiokoa ndipo nikaokoa wengine kwa kutoboa paa la nyumba, niliokoa wanawake na watoto. Sijawahi kushukudia hali kama hii katika maisha yangu,” anasema.
“Nilipishana na maiti kama mbili na sikuhangaika kuziopoa kwa sababu nilitaka kuwaokoa waliokuwa hai?" anasimulia.
Simon amepoteza ndugu na jamaa aliokuwa nao katika biashara, bado anaonekana mwenye kujawa na mawazo. “Achana na mali kwani zinapatikana kwa mazingira yeyote, je furaha iko wapi kama huna watu? Furaha ni watu,” anasema huku akifuta machozi.
Baadhi waliiambia TRT Afrika kwamba kumbukumbu za tukio hilo kamwe haziwezi kuwatoka mapema akilini.
Serikali imesema chanzo cha janga hilo ni kumeguka kwa sehemu ya mlima Hanang yenye miamba dhoofu iliyonyoya maji ya mvua na kuporomoka na hivyo kutengeneza tope.
Vikosi vya kupambana na maafa vinaendelea kuondoa tope mitaani na barabarani, kufukua mali na nyumba kwenye tope na kutafuta iwapo bado kuna miili iliyonaswa katika tope hizo.
Wakati huo huo, serikali imesema italipia gharama zote za mazishi ya watu zaidi ya 60 waliopoteza maisha yao katika maporomoko hayo, pamoja na kulipia gharama za waliojeruhiwa ambapo mpaka wanapata matibabu katika hospitali mbalimbali ikiwemo ile ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.
Wataalamu wa maafa wanakiri kwamba, hali kama hii haijawahi kutokea kwa miongo kadhaa. Hata hivyo, wengi wanasema, kutokea kwa janga hili ni sehemu tu ya athari zinazojitokeza katika maeneo mbalimbali za mabadiliko ya tabia nchi.
Katika kipindi cha miezi kadhaa nchini Tanzania, Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini humo ilitangaza kuwepo kwa mvua za El Nino na kuwataka kuchukua tahadhari.
Mbali na Tanzania, baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya na Somalia tayari zimeshuhudia madhara makubwa yatokanayo na mvua hizo, ikiwemo vifo, pamoja na uharibifu wa makazi na miundombinu muhimu.
Madhara haya, yanatokea wakati wakuu mbalimbali wa nchi pamoja na viongozi kutoka taasisi na mashirika ya mazingira wakiwa mjini Dubai, UAE, kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi, COP28.