Ronald Sonyo
TRT Afrika, Katesh, Tanzania
Vifo vya zaidi ya watu 79 wilayani Hanang Mkoani Manyara nchini Tanzania vimeacha makovu yasioweza kufutika hasa kwa wale waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki kutokana na maporomoko yaliyotokea katika eneo hilo. Hii ni mbali na hasara ya uharibifu wa mali na mifugo.
Ni tukio lililogusa hisia za wengi na kuwaacha wengine kama vile Simon Ngaida na upweke usioelezeka. Hii ni baada ya kupoteza wana familia 12.
Kama wasemavyo wahenga, mtu ajua atokako, hajui aendako, na hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Simon. Aliiaga familia yake akielekea Mkoani Tanga kikazi, lakini siku moja tu baada ya kuondoka huku nyuma maporomoko yalisambaratisha maisha ya familia yake na kuzima ndoto yake ya maisha.
“Nilikwenda Tanga kikazi, lakini nilipofika tu nikaambiwa familia yangu imepata matatizo. Tumepata miili 12 na mtoto wangu amepatikana akiwa mahututi na sasa yupo hospitali. Mwanangu mmoja sijampata, namuomba Mungu nimuone walau akiwa hai ama amekufa, lakini nakaribia kukata tamaa,” alisema Simon huku akivuta pumzi kwa nguvu.
“Nimeathirika sana na sijui namna ninavyoweza kueleza,” anakohoa kisha anaendelea, "Namuomba Mungu nimpate mwanangu, sina jinsi na ninaomba serikali iendelee kutusaidia,” amesema Simon.
Simon anawakilisha nyuso za wengi waliokata tamaa kufuatia mafuriko hayo. Usiku wa wa kuamkia leo katika viunga vya mji, nilijionea watu wakiwa wameshikana mikono kwa pamoja, makundi kwa makundi kama njia ya kujihami kutokana na tope ambazo zimezagaa mitaani.
Hali hii ilifuatiwa na mvua kubwa ilioendelea kunyesha kwa saa kadhaa na kusababisha maji kujaa katika baadhi ya maeneo na hata nyumba za watu kumezwa.
Hata hivyo, tangu kutokea kwa janga hilo, kazi kubwa inayofanywa na wakazi wa maeneo yaliyoathirika ni kuhamisha tope na kujaribu kurudisha hali kama kuonekana kama ilivyokuwa.
Alipotembelea eneo hilo, rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliwataka wakuu wa mikoa kujiweka katika hali ya tahadhari na kuhakikisha kunakuwa na akiba ya chakula wakati majanga yanapotokea.
Pia aliagiza kufanyika kwa uchunguzi wa mali zilizoathirika, mifugo na maeneo yanayopaswa kuhamishiwa watu wanaoishi katika mazingira hatari pamoja na watalamu kuendelea na uchunguzi wa kupata kiini na kina cha janga hilo.
Baadhi walieleza kuwa hotuba ya rais Samia imewapoza makovu, lakini baadhi wanatamani walau wajengewe makazi mapya, huku wakionyesha hofu ya kurudi katika eneo hilo.
"Tunataka tuhame moja kwa moja. Hii ni ajali kubwa. Nimepoteza watoto watano na mke, amebakia kijana mmoja tu, sasa nitaweza vipi kurudi hapa," amesema Paulo Elias, mkazi wa Katesh.
"Mwaka 2011, ilitokea hali ya namna hii, lakini hatukuogopa sana kwa sababu haikuwa kwa kiwango kikubwa kama hivi. Sasa mwaka huu, inapokuwa kwa kiwango kikubwa kama hiki, huenda tukawa na mashaka kwamba inaweza kutokea tena, na kama itachukua miaka mengine, hatutashauri watoto na wajukuu waendelee kuishi maeneo kama haya. Labda watafute sehemu nyengine," anasema Samweli Mtinda, mkazi wa Katesh.
Kulingana na kitengo kinachoshulikia maafa nchini Tanzania, hakukua na tetemeko la ardhi wala mlipuko wa volcano, kama ilivyokuwa ikidaiwa hapo awali, bali wataalamu wanasema kilichotokea ni mmegeko wa sehemu ya mlima huo wenye miamba dhoofu iliyonyoya maji ya mvua na kuporomoka (landslide) na hivyo kutengeneza tope (mudflow).
Awali Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania ilitahadharisha kutokea kwa mvua za El Nino na hivyo kuwataka wananchi katika maeneo mbalimbali nchini humo kuchukua tahadhari ikiwemo kukaa katika maeneo salama.
Mbali na Tanzania, mvua hizo pia zimeleta madhara katika maeneo mengine ya Afrika Mashariki ikiwemo Mashariki na Kaskazini mwa Kenya, pamoja na Somalia ambapo watu kadhaa wamepoteza maisha, huku wengine wakiachwa bila makazi. Wataalamu wa masuala ya hali ya hewa wanasema hizo ni baadhi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi.