Ronald Sonyo
TRT Afrika, Katesh, Tanzania
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewasili katika mji mdogo wa Katesh Mkoani Manyara kujionea hali halisi na kiwango cha madhara kilichotokea baada ya mafuriko kuvikumba baadhi ya vijiji katika eneo hilo.
Mara tu baada ya kuwasili, rais Samia ametembelea kata ya Jorodom, ambayo ni miongoni mwa maeneo yaliyokumbwa na mafuriko. Baadae kiongozi huyo wa nchi ambae aliongozona na viongozi wengine ikiwemo wale wa Mkoa wa Manyara alitembelea majeruhi katika Hospital ya Wilaya, Tumaini kabla ya kwenda kambi inayotumika kuhifadhi waathirika wa maafa hayo.
Alitoa pole kwa waathirika na kusema Serikali ipo pamoja nao katika kipindi hiki cha maafa.
Janga hilo lilivikumba vitongoji vya karibu vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay na Sebasi, wilayani Hanang, Mkoani Manyara.
Wakati huo huo, maiti mbili zimeopolewa kutoka katika tope zilizotokana na maporomoko hayo ambayo mpaka sasa yamesababisha vifo vya watu 69, kwa mujibu wa serikali.
Kati ya maiti hizo mbili, moja ni ya mtoto mwenye umri wa miaka tatu.
Awali baba wa mtoto huyo, wakati akizungumza na waandishi wa habari, alisema angetamani kumpata mtoto wake.
"Natamani kumpata mwanangu awe hai ama amekufa, lakini natamani kumuona," alisema.
Ingawa hali ya maumivu ipo, lakini kuna faraja kwamba idadi kubwa ya waliopotea wamepatikana.