Hija ya 2023 inasemekana kuwa kubwa zaidi baada ya miaka mitatu ya vikwazo vya Uviko-19. Saudi Arabia ilitarajia zaidi ya watu milioni mbili kuhudhuria.
Mahujaji wa Kiislamu wamefika katika mlima Arafat nchini Saudi Arabia ikiwa ndicho kilele cha ibada ya hija ya kila mwaka.
Hapa waumini husoma aya za Qur'an, pamoja na kuomba dua za kutubia na kumtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi, kuambatana na mafundisho ya dini, Hapa ni eneo ambapo inaaminika kuwa mtume Muhammad alitoa hotuba yake ya mwisho.
Kufanya ibada katika Mlima Arafat ni sehemu ya lazima ya hija. Ni mojawapo ya shughuli zenye changamoto nyingi za kimwili na imani pamoja na kiakili.
Mahujaji husali kwa saa kadhaa na kusoma Quran kwenye Mlima Arafat na katika maeneo yanayozunguka kwa kawaida huku kukiwa na joto kali.
Hali ya joto ilipanda hadi nyuzijoto 46 siku ya Jumatatu huku waumini waliojikinga kwa miavuli wakisafiri kutoka Mecca hadi Mina, ambako walilala katika mojawapo ya miji mikubwa ya mahema duniani, kabla ya ibada katika Mlima Arafat siku ya Jumanne.
Wakati wa kuzama kwa jua mahujaji husafiri umbali mfupi kutoka Mlima Arafat hadi Muzdalifah, eneo katikati ya Arafat na Mina, ili kulala kwenye eneo wazi.
Baada ya Arafat, mahujaji hukusanya kokoto ili zitumike katika ibada ya kupigwa mawe kwa nguzo zinazoashiria shetani huko Mina.
Hija ni kitendo cha kiroho muhimu sana kwa mahujaji ambao wanaamini huondoa dhambi, huwaleta karibu na Mwenyezi Mungu na pia kuwaunganisha Waislamu wapatao bilioni mbili duniani.
Wengine hutumia miaka mingi kuweka akiba ya pesa na kusubiri kibali cha kuanza safari hii.
Mwaka huu, vizuizi vya Uviko-19 vimeondolewa bila kulazimika kuwepo na umbali wa kijamii na kuvaa barakoa. Kikomo cha juu cha umri wa miaka 65 pia kimeondolewa.
Hii imewapa maelfu ya wazee fursa ya kuhudhuria Hija ambayo inahitajika kwa Waislamu kutekeleza angalau mara moja katika maisha yao.
Hija ni mojawapo ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini ulimwenguni. Inawaleta pamoja Waislamu - vijana kwa wazee, matajiri kwa maskini - kutoka duniani kote.
Baada ya Arafat na kurusha mawe, kituo cha mwisho ni kurejea kwenye Msikiti Mkuu wa Mecca, ambapo Waislamu wanafanya mzunguko wa mwisho wa Kaaba, mchemraba mkubwa mweusi ambao Waislamu ulimwenguni kote husali wakielekea ilipo kila siku.
Wakati wa ibada ya Hija, wanaume wote wanatakiwa kuvaa mavazi meupe meupe bila ya kushonwa, sheria inayolenga kuashiria usawa wa matajiri na masikini kumtukuza Mwenyezi Mungu.
Wanawake lazima waache bidhaa za urembo na wafunike nywele zao lakini wana uwezo zaidi ya kuvaa vitambaa kutoka nchi zao za asili, na hivyo kufanya maonyesho ya rangi, ya tamaduni nyingi za kiislamu.
Mamlaka ya Saudia imetoa helikopta zinazozunguka angani kwa ufuatiliaji na maelfu ya wafanyikazi wa afya na ambulensi kuhudumia dharura za matibabu.
Kutokana na hali ya hewa kuwa joto sana, mahujaji wengi mara nyingi huchagua kofia za majani yenye ukingo mpana na miavuli ya kila rangi ni ya kawaida.
Mwishoni mwa Hajj, sikukuu ya Eid al Adha huadhimishwa na Waislamu duniani kote.
Kwa wale ambao wanaweza kumudu, wanatarajiwa kuchinja mifugo kama kondoo, ng'ombe na ngamia kama kafara na kisha kugawa sehemu ya nyama kwa maskini.