Upasuaji wa kuwatenganisha mapacha walioungana kutoka Tanzania waanza nchini Saudi Arabia. Picha: SPA

Hatimaye upasuaji wa kuwatenganisha watoto mapacha waliozaliwa nchini Tanzania wakiwa wameungana Hassan na Hussein Omari Saidi, umeanza rasmi nchini Saudi Arabia. Upasuaji huo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu, kwa mujibu wa wataalamu wanasema utachukua takriban siku nzima kukamilika.

Zoezi hilo la upasuaji linaanza baada ya miezi kadhaa ya uchunguzi wa kina uliosimamiwa na watalaamu mbalimbali wa afya ya watoto katika Hospitali Kuu ya Watoto ya Mfalme Abdullah mjini Riyadh.

Daktari Abdullah Al Rabeeah ambaye ni mshauri katika Mahakama ya Kifalme na Msimamizi Mkuu wa kituo cha Msaada wa Kibinadamu cha Mfalme Salman (KSRelief) ndiye anawaongoza watalaam katika upasuaji huo. Watoto hao wana umri wa miaka miwili na uzito wa kilo 13.5 kwa pamoja.

Hassan na Hussein, Mapacha wa Tanzania wakiwa kwenye chumba cha upasuaji. Picha: TRT Afrika Swahili 

Katika mkutano na waandishi wa habari, Dk. Al Rabeeah alisema kuwa upasuaji huo unatarajiwa kuchukua masaa 16 na utafanywa kwa awamu tisa na jopo la madaktari 35, wataalamu na wafanyakazi wa kiufundi na wauguzi.

"Uchunguzi wa kimatibabu ulifanywa mara nyingi na iligunduliwa kwamba mapacha hao wanatumia pamoja sehemu ya chini ya kifua, tumbo, na nyonga, na kila mmoja ana kiungo kimoja cha chini, na wana kiungo cha chini cha tatu kilichoharibika. Pia wameungana kwenye ini, matumbo, mfumo wa mkojo, na kuwa na kiungo kimoja cha uzazi cha kiume, na zimedhoofika katika ukuta wa chini wa tumbo na kibofu cha mkojo," amesema Dk. Al Rabeeah.

Katika mahojiano maalumu na TRT Afrika Swahili, Dk. Zaituni Bokhari, ambae ni maarufu kwa upasuaji wa watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, iliyopo jijini Dar es Salaam, Tanzania, ambaye amekuwa na watoto hao kwa muda mrefu, amethibitisha kwamba watoto hao wameingia chumba cha upasuaji mapema leo huku shughuli hiyo ikiongozwa na madaktari wa Saudi Arabia.

Mapacha hao ambao waliwasili nchini Saudi Arabia mwezi Agosti wakiwa pamoja na mama yao. Picha: TRT Afrika Swahili

Kabla ya kuwasilini nchini Saudi Arabia mwezi Agosti mwaka huu, watoto hao, walikuwa wakihudumiwa katika Hospitali ya Muhimbili kwa takriban miaka miwili. Hassan na Hussein walizaliwa magharibi mwa Tanzania.

Dk. Zaituni amesema uhusiano bora wa nchi mbili hizo ndio uliofanikisha kufanyika kwa upasuaji huo.

"Nawaomba Watanzania na watu wote wawaombee malaika hawa, waweze kufanyiwa upasuaji kwa kheri. Kwa hakika upasuaji wa kuwatenganisha si jambo rahisi lakini tuna imani watatoka salama," Dk. Zaituni ameiambia TRT Afrika Swahili.

Wakati huo huo, mtaalamu huyo bingwa wa upasuaji ameushukuru uongozi wa Hospitali ya Muhimbili kwa kuwapokea watoto hao tangu wakiwa na wiki moja na kuwasimamia ipasavyo kwa muda wa takriban miaka miwili mpaka waliposafirishwa kwenda nchini Saudi Arabia.

Mpango wa Saudi Arabia wa kutenganisha mapacha waliounganishwa, umekuwa ukiendelea kwa kipindi cha miaka 33 iliyopita, huku ukifanikiwa kuwatenganisha mapacha 58 waliounganishwa.

TRT Afrika