Kikosi cha RSF nchini Sudan (RSF) kimesema kimechukua uwanja wa ndege kutoka kwa jeshi, Magharibi mwa mji mkuu na wafanyikazi katika uwanja wa mafuta walisema walihamishwa kutokana na shambulio hilo huku pande zinazozozana zikikutana tena kwa mazungumzo nchini Saudi Arabia.
RSF ilitangaza Jumatatu kuwa uwanja wa ndege wa Belila katika jimbo la Kordofan Magharibi ulikuwa ukitumiwa na jeshi, ambalo limekuwa likipigana tangu katikati ya mwezi wa Aprili 2023, kurusha ndege za kivita.
Uwanja wa Belila, ulioko kilomita 55 Kusini Magharibi mwa Al-Fula, mji mkuu wa Jimbo la Kordofan Magharibi, ni makao ya uwanja wa mafuta ambao, kabla ya kuzuka kwa vita, ulikuwa ukizalisha makumi ya maelfu ya mapipa ya mafuta kila siku. Hata hivyo, uzalishaji umetatizwa sana katika kipindi cha miezi saba iliyopita.
Wahudumu katika uwanja wa mafuta wa Belila, ambao huzalisha sehemu kubwa ya mafuta duni inayozidi kupungua Sudan, walisema walihamishwa Jumapili usiku kwa sababu ya mapigano hayo.
Hata hivyo, RSF ilisema katika taarifa yake kwamba itaruhusu uwanja wa ndege na eneo la mafuta kuendelea kufanya kazi.
Jeshi la Sudan na wizara ya mafuta haijatoa kauli mpaka sasa.
Pande hizo mbili pia zimekuwa zikipigana katika miji ya Magharibi ya El Obeid na El Fasher katika siku za hivi karibuni, huku mazungumzo yanayodhaminiwa na Marekani na Saudi Arabia ambayo yanalenga kusuluhisha usitishaji vita wa kudumu, yakianza tena Jumapili katika mji wa Jeddah, Saudi Arabia.
Wakati huo huo, siku ya Jumatatu, kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ilisema imewezesha kuachiliwa kwa wanajeshi 64 waliokuwa wamezuiliwa na RSF, na kufanya jumla ya watu walioachiliwa wakati wa vita kufikia hadi 292.
RSF, ambayo ina ngome yake kuu huko Darfur, imekuwa ikipigania kupata udhibiti wa miundombinu muhimu magharibi mwa nchi katika juhudi za kusitisha operesheni za jeshi.
Wiki iliyopita, ilisema kuwa imeteka Nyala, mji wa pili kwa ukubwa nchini Sudan na mji mkuu wa Darfur Kusini.
Mkazi mmoja wa Nyala alisema jeshi limeendelea na mashambulizi ya anga hata wakati RSF ilipokuwa ikichukua kambi yake kuu mjini humo.