Wadau wa elimu Tanzania wataka hatua stahiki kudhibiti udanganyifu kwenye mitihani

Wadau wa elimu Tanzania wataka hatua stahiki kudhibiti udanganyifu kwenye mitihani

Hii inafuatia maaumuzi ya Baraza la Mitihani Tanzania kufuta matokeo ya watahiniwa zaidi ya 200.
Watahiniwa wakiwa ndani ya chumba mitihani.

Wadau wa elimu nchini Tanzania wamezitaka mamlaka husika kuchukua hatua stahiki dhidi ya udanganyifu unaofanywa na wanafunzi wakati wa mitihani.

Hatua inakuja baada ya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kubatilisha matokeo ya wanafunzi zaidi ya 200 kwa tuhuma za udanganyifu wakati wengine walipatikana wakiwa wameandika matusi katika karatasi maalumu za kujibia mitihani.

Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa NECTA, Dkt Said Mohamed alisema watahiniwa 178 waliofanya mitihani ya kujipima uwezo ya darasa la nne, wakati wengine 28 wa kidato cha nne walifutiwa matokeo yao kutokana na tuhuma hizo.

''Nia ni kurejesha uaminifu katika usimamizi wa mitihani ya taifa,'' alinukuliwa akisema.

Hii sio mara ya kwanza kwa watahiniwa kufanya udanganyifu na kuandika mambo yasiofaa kwenye mitihani yao.

Mwaka juzi, baadhi ya karatasi za majibu zilipatikana na michoro ya vikaragosi na baadhi kuandikwa nyimbo zisizofaa kwenye maadili ya Kitanzania.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na TRT Afrika, wadau wa elimu Tanzania wamekemea vitendo vya aina hiyo, huku wakielekeza lawama kwa mamlaka za elimu kushindwa kuchukua hatua stahiki mapema.

''Kwa bahati mbaya sana tuko makini kuchukua hatua za haraka kutibu makosa ya namna hii, kuliko kutafuta muarobaini wake,'' anaeleza Nicodemus Shauri, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyokuwa ya Serikali ya Maarifa ni Ufunguo, nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Shauri, kuna viashiria kwamba tatizo hili ni kubwa sana, tofauti na mamlaka za elimu zinavyofikira.

Mtaalamu huyo wa Elimu anaweka bayana kuwa wanafunzi kutoka shule za umma ndio wanaohusika zaidi kwenye matendo ya namna hii.

Shauri anakwenda mbali zaidi na kudai kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wa shule za umma, wamekata tamaa na elimu, hasa ukizangatia wapo kwenye mazingira duni kuliko wale wanaotoka shule za binafsi.

''Mazingira waliyonayo yanawafanya kutojali hata umuhimu wa mitihani wanayofanya, kwao ni bora liende tu,'' anaongeza.

Maoni ya Shauri yanaungwa mkono na Benjamin Masebo, Afisa Utafiti kutoka Shirika la Uwezo Tanzania.

Masebo anasema hali duni na isiyoridhisha kwenye shule za umma zinapelekea watahiniwa kutoka taasisi hizo kufanya mizaha yenye kuwagharimu.

''Ni wakati muafaka sasa kuongeza hamasa ya ufundishaji kwenye shule za umma, hii ina maanisha kuwapa motisha walimu na wanafunzi ili wafurahie maisha yao ya shule,'' anaeleza.

Ni imani ya Masebo kuwa kufuta matokeo ya watahiniwa sio muarobaini sahihi wa tatizo lililopo.

Anasema, "Sidhani kama kuwafutia matokeo ni utatuzi sahihi; hata ule udanganyifu unaanzia kwa watu wazima na sio watoto. Tukae chini na watoto, tujue kwa nini wanadanganya kwenye mitihani."

Kwa upande wake, Ambrose Akyoo mzazi na mkazi wa Arusha, Tanzania, ameiomba serikali kuweka utaratibu madhubuti utakaoondoa mianya yoyote ya udanganyifu wakati wa mitihani.

''Ni ukweli usiopingika kwamba udanganyifu wa aina yoyote kwenye mitihani kwa ngazi yoyote haukubaliki, hivyo hatua lazima zichukuliwe. Lakini hatua hizo na adhabu zinatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kiweka mizani sawia. Ipo mifano kadhaa ya shule ambazo zimefutiwa matokeo yake na hata wazazi, walezi pamoja na wanafunzi waliofutiwa kubaki na mshangao,'' ameongeza.

TRT Afrika