Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dkt Said Mohamed./Picha: @NectaTz

Kiwango cha ufaulu kwa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne kimepanda hadi kufikia asilimia 92.37 kutoka asilimia 89.36, Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limesema Januari 23.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa NECTA Dkt Said Mohamed, kiwango cha ufaulu kwenye mitihani hiyo kimeongezeka kwa asilimia 3.01.

“Wakati wavulana wamefaulu kwa kuwango cha asilimia 93.72, wasichana walifikia asilimia 91.72,” alisema Dkt. Mohamed wakati akitangaza matokeo hayo Januari 23, 2025.

Kulingana na NECTA, idadi ya watahiniwa waliopata madaraja I, II, na III mwaka 2024 imeongezeka hadi 221,953 ambayo ni sawa na asilimia 43 ikilinganishwa na 197,426, sawa na asilimia 37.4 mwaka 2023.

Aidha, idadi ya waliopata daraja la IV na sifuri imepungua, ikionyesha ubora wa ufaulu kuongezeka kwa asilimia 5.6.

Wakati huo huo, Baraza hilo limefuta matokeo yote ya watahiniwa 67 waliobainika kufanya udanganyifu na Watahiniwa watano walioandika lugha ya matusi katika skripti zao katika mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba 2024 ambapo matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 (2) (j) cha Sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 30(2) (b) cha Kanuni za Mitihani Mwaka 2016.

TRT Afrika